Simba yaanzisha mfumo wa Ulaya

Wachezaji wa timu ya Simba wakimsikiliza kocha wao, Abdallah Kibadeni katika kambi yao bamba beach jijini Dar es Salam,
Muktasari:
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema: “Kuna programu mpya kwenye timu, itasaidia kutoa changamoto kwa wachezaji kwani wote watahitajika kucheza kwa kiwango cha juu ili kubaki kwenye kikosi cha kwanza na cha pili.”
SIMBA imeanza mambo ya Ulaya. Benchi la Ufundi limetoa utaratibu mpya wa kuingiza timu kambini kulingana na mchezo husika na watakaoshindwa kuonyesha viwango watacheza mechi maalumu nje ya kambi.
Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema: “Kuna programu mpya kwenye timu, itasaidia kutoa changamoto kwa wachezaji kwani wote watahitajika kucheza kwa kiwango cha juu ili kubaki kwenye kikosi cha kwanza na cha pili.”
“Wachezaji wanaojitambua na kulishawishi benchi la ufundi kwa kiwango, wataingia kambini, hawatazidi wachezaji 26 kambini kwani nataka vita ya namba na pia itakuwa kama tahadhari kwa wachezaji wazembe na wasiojielewa.
“Hatutataka uzembe kwenye kazi, kila mchezaji anajua kazi yake hivyo mafanikio ndiyo yanayohitajika ili timu ijivunie ilichokipanda,” alisema Kibadeni na kuongeza kuwa wachezaji ambao hawataingia kambini watafanya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Kinesi chini ya kocha msaidizi na watakuwa na mechi maalumu kila Alhamisi na atakayeonyesha kubadilika atarudishwa kikosi cha kwanza. Wachezaji 26 walioingia kambini kwa wiki moja katika Hoteli ya Bamba Beach, Kigamboni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ni Abel Dhaira, Tambwe Amisi, Gilbert Kaze, Amri Kiemba, Haruni Chanongo, Jonas Mkude, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ Henry Joseph, Nasoro Masoud ‘Chollo’, Miraj Adam, Miraji Athumani, Ramadhan Chombo ‘Redondo’, Said Ndemla na Betram Mwombeki.
Wengine ni Andrew Ntalla, Ramadhani Singano ‘Messi’, Hassan Khatibu, Rahim Juma, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ , William Lucian, Sino Agustino, Ibrahim Twaha ‘Messi’, Zahoro Pazi, Abou Hashim, Adeyoun Saleh na Rashid Mkoko.
Wachezaji ambao hawakuingia kambini kwa ajili ya mchezo wa huo ni Joseph Owino (aliyekuwa mgonjwa), Haruna Shamte (nahodha msaidizi), Abdallah Seseme, Hassan Isihaka, Marcel Kaheza, Edward Christopher, Omary Salum, Emil Mgeta na Frank Sekule.