Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yaamua kiume

Muktasari:

Viongozi hao wameamua kiume kwa kuanza msako wa wachezaji wapya wa kigeni na kuanza mchakato wa kuwatema wachezaji wote walioonekana mzigo katika klabu hiyo mpaka sasa Ligi Kuu ikiingia raundi ya tisa

BAADA ya kujishtukia kuwa imechemka sana kwenye usajili wa msimu huu, klabu ya Simba imeamua kufanya kwelina kama mipango yao itakaa vyema na kufanikiwa, basi ni lazima wapinzani wao wa Ligi Kuu Bara waombe po!

Viongozi wa Simba wamejawa na hasira baada ya kuzishuhudia Yanga na Azam zikifanya vyema kwenye mechi zao za Ligi Kuu Bara, huku straika wao ngongoti, Pape N’Daw kutoka Senegal akifanya kituko ambacho kimeiacha klabu hiyo katika aibu kubwa mbele ya wadau wa soka.

Pape N’Daw anatuhumiwa kukutwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni hirizi wakati wa pambano lao lililopita la ligi dhidi ya Prisons lililochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na Simba ilichezea kichapo cha bao 1-0.

Viongozi hao wameamua kiume kwa kuanza msako wa wachezaji wapya wa kigeni na kuanza mchakato wa kuwatema wachezaji wote walioonekana mzigo katika klabu hiyo mpaka sasa Ligi Kuu ikiingia raundi ya tisa.

Hatua hiyo imekuja siku chache kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa na majina sita ya wachezaji wa kigeni wamependekezwa kusajiliwa Msimbazi, huku waliopo sasa akiwamo Pape N’Daw, Simon Sserunkuma, Vincent Angban wakiwa mashakani.

Raphael Kiongera anayecheza kwa mkopo KCB Kenya ni kati ya wachezaji watakaovaa uzi wa Wekundu wa Msimbazi wakati Ligi Kuu ikirejea tena kuchezwa kutoka mapumzikoni.

Kiongera ana nafasi kubwa ya kurejea Simba ingawa mapenzi yake ya kuchezea klabu hiyo yanaonekana kupungua huku KCB ikielezwa kuendelea kuhitaji huduma yake ila atalazimika kurudi kwa sababu ana mkataba na klabu hiyo. Mkataba wa Kiongera utamalizika Agosti, 2016.

Wengine

Achana na habari za Kiongera. Simba inayohitaji kusajili winga mmoja, mastraika wawili, beki wa kushoto na wa kati imewaweka kwenye mipango ya usajili wachezaji kadhaa na Mwanaspoti inayo orodha ya majina yao na klabu wanazotoka.

Wachezaji hao ni Laudit Mavugo ambaye alikoswakoswa kusajiliwa usajili uliopita kutokana na dau kubwa iliyokuwa ikitaka klabu yake ya Vital’O ya Burundi anaomaliza nao mkataba, pia kuna Erisa Ssekisambu na Farouk Miya wote wakitokea Vipers ya Uganda.

Straika mwingine ambaye yupo kwenye rada za Simba ni Edmore Chirambadare wa Chicken Inn ya Zimbabwe ambaye anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu ya huko akiwa na mabao 11 na viongozi wa Simba wamekuwa wakimfuatilia na kuanza mchakato na klabu yake, ingawa dau linalohitajika ili kumng’oa alipo linaweza kuwakimbiza mabosi hao wa Msimbazi.

Wengine wanaopigiwa hesabu na Simba ni winga Brain Majengwa ambaye suala lake bado lipo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baina yake na Azam FC na Kelvin Ndayisenga ambaye usajili wake ulishindikana dakika za mwishoni na mchezaji huyo raia wa Burundi alishindwa kurudi kusaini mkataba baada ya kufikia makubaliano na wakala wake na ikawa sababu ya Simba kumsajili N’daw ambaye alisajiliwa kwa mkopo wa miezi mitatu.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa wachezaji watatu wa kigeni wataachwa ili kupisha wengine watatu watakaoingia. Watakaoachwa ni Sserunkuma na N’Daw, huku Emiry Nimubona akitajwa kupelekwa kwa mkopo katika moja ya timu watakayomtafutia.

Mpaka sasa Simba ina wachezaji saba wa kigeni ambao ni kipa Vincent Angban, Emiry Nimubona, Juuko Murshid, Simon Sserunkuma, Hamis Kiiza, Justice Majabvi na Pape N’daw.

Hata hivyo, kama Simba itasajili wachezaji watatu basi nafasi moja itakuwa ni ya Kiongera ambaye imedaiwa kuwa mmoja wa viongozi anatarajia kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kumfuata mshambuliaji huyo ambaye mkataba wake wa mkopo unamalizika Novemba 15.

Mwanaspoti limedokezwa kuwa Mavugo ana asilimia kubwa ya kujiunga na Simba kwani mkataba wake unamalizika Desemba, hivyo atakuwa mchezaji huru, Erisa ana mkataba wa miaka mitatu na timu yake, hivyo Simba kama inamhitaji italazimika kuvunja mkataba huo.

Kwa upande wa Chirambadare imeelezwa fedha anayohitaji ni nyingi na ametaka alipwe Dola 5000 kwa mwezi kama mshahara wake wakati ndani ya Simba hakuna mchezaji anayelipwa mshahara unaozidi Dola 1500 kwa sasa, hivyo usajili wake unaweza kuachwa.

Wazawa

Pia chanzo hicho kilisema kuwa kwa upande wa wachezaji wazawa, Ibrahim Ajibu na Issa Abdallah watapelekwa kwa mkopo. Imeelezwa kuwa sababu ya Ajibu kupelekwa kwa mkopo ni kushuka kwa kiwango chake huku Issa ni kwenda kupata uzoefu kwani hapati namba kwa sasa.

“Wote hao wako kwenye mipango, siyo lazima tuwasajili wote, tunaangalia wapi pana unafuu na inawezekana kwa haraka, kwani shida yetu ni kupata mastraika wawili, winga, beki wa kulia na wa kati ambao viwango vyao vinastahili kuichezea Simba kwa mafanikio,” kilisema chanzo chetu.

“Inawezekana pia yakaletwa majina mengine zaidi ya hayo na tutaangalia uwezo wa mchezaji husika.”

Simba inahitaji kusajili beki wa kulia ambaye atampa changamoto Hassan Kessy na beki wa kati atakayempa ushindani Hassan Isihaka ingawa yupo Mohammed Fakhi ambaye bado hajaaminiwa katika kikosi hicho.

Katika safu ya ushambuliaji kama hakutakua na tatizo itaendelea kuwategemea zaidi Mussa Mgosi, Kiiza na Geofrey Maganga.