Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba ya Moro mtashika adabu

Nyota wa Simba wakijifua kwenye mazoezi yao yanayoendelea mjini Morogoro, kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. PICHA|DORIS MALIYAGA

Muktasari:

  • Kinachoonekana kambini Morogoro ni mpira mwingi wa Mwanjali ambaye anacheza pia katika timu ya taifa ya Zimbabwe jambo lililomfanya Omog kuwaweka kando Novatus Lufungo na Emmanuel Semwanza katika eneo hilo.

KOCHA wa Simba, Joseph Omog ameiona ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu ujao na kugundua kuwa ana siku 30 tu za maandalizi ya mwisho kabla ya msimu kuanza na kuamua kufanya kazi moja kubwa ya haraka ambayo ni kupata kikosi kipya cha kwanza cha timu hiyo ambacho Agosti 20 tu kitaifundisha adabu Ndanda FC hapo taifa halafu wengine wajipange.

Kwa haraka Omog ameanza kuzifanyia kazi nafasi nne ambazo zimeachwa wazi na nyota walioondoka na mbili ambazo wachezaji waliopo sasa hawazimudu vizuri. Nafasi hizo ni beki ya kulia, beki ya kati, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji, straika na winga ya kushoto hivyo kupata mwonekano mpya wa kikosi cha kwanza kinachotarajiwa kufanya makubwa. Wachezaji watano wapya; beki wa kulia, Hamad Juma, beki wa kati Method Mwanjali raia wa Zimbabwe, kiungo Mdhamiru Yassin na washambuliaji Blagnon Frederick na Shiza Kichuya tayari wamepewa nafasi katika kikosi hicho lakini Omog ametahadharisha kuwa nyota yeyote mpya mkali na ambaye atakaza buti mazoezini anaweza kupangua kikosi.

Kinachoonekana kambini Morogoro ni mpira mwingi wa Mwanjali ambaye anacheza pia katika timu ya taifa ya Zimbabwe jambo lililomfanya Omog kuwaweka kando Novatus Lufungo na Emmanuel Semwanza katika eneo hilo.

Beki huyo ambaye kama atapewa mkataba atakuwa Mzimbabwe wa kwanza anayecheza nchini ambaye ana nafasi katika timu yao ya taifa na kuwapiku Donald Ngoma na Thaban Kamusoko ambao hawana hata nafasi kwenye benchi la timu hiyo, anasifika kwa uwezo mkubwa wa kuziba nafasi, kukaba mtu na mtu na kucheza mipira ya juu.

Hamad Juma tayari amepewa mikoba ya Hassan Kessy ambaye alitimkia Yanga na ameanza kupewa mafunzo makali ili kuendana na kasi ya Omog ambaye miongoni mwa mipango yake ya muda mfupi ni kuhakikisha Simba inarejesha heshima yake nchini.

Katika eneo la safu ya kiungo wa chini kwa sasa Omog amempa kazi hiyo Mdhamiru Yassin ambaye hata hivyo anatarajiwa kucheza zaidi kama kiungo mshambuliaji na kumuachia nafasi hiyo Jonas Mkude ambaye amekwenda kufanya majaribio nchini Afrika Kusini.

Awali Omog alikuwa akimjaribu Mkongomani Mussa Ndusha kama kiungo mshambuliaji lakini kuna taarifa kuwa huenda Mkongo huyo akaungana na mwenzie Besele Bokungu ambaye tayari amefungashiwa virago.

Masharti yaliyotolewa na mabosi wa Simba ni kuwa wachezaji wote wa kigeni lazima waanze katika kikosi cha kwanza vinginevyo nafasi zao wasajiliwe tu wachezaji wazawa.

 Shiza Kichuya amekabidhiwa winga ya kushoto na anaonyesha uwezo mzuri mazoezini jambo ambalo litamfanya nahodha wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mgosi’ kuendelea kusugua benchi huku Peter Mwalyanzi akisubiria kudra za mwenyezi Mungu kufahamu hatma yake.

Muivory Coast, Blagnon Frederick tayari amekabidhiwa nafasi ya Kiiza na sasa Omog ameanza kumuongezea makali ili aweze kufunga kwa njia nyingi zaidi ikiwemo kwa mipira ya krosi na kona kwa kutumia faida ya urefu wake jambo ambalo tayari limeanza kufanikiwa. Mabadiliko hayo mpaka sasa yanawapa nafasi wachezaji watano tu wa zamani katika kikosi hicho ambao ni kipa Vincent Angban, mabeki Mohammed Hussein na Juuko Murshid pamoja na kiungo Mwinyi Kazimoto na mshambuliaji Danny Lyanga.

NDEULE ATUA

Beki Malika Ndeule mwenye uwezo wa kucheza namba za pembeni kama mbili na tatu, aliwahi kufanya kazi na kocha wa sasa wa Simba, Joseph Omog kwenye kikosi cha Azam ambacho kilichukua ubingwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014.

Jana Alhamisi Ndeule alitua kwenye kambi ya timu hiyo na kujifua mazoezini na wenzake  waliotangulia mapema mjini hapa.

Uamuzi wa Omog kumchukua Malika umekuja baada ya kuona kikosi chake hakijakaa vema kwenye beki mbili, ambapo aliagiza mabosi wake wawatafute wachezaji wenye sifa hizo ili ligi itakapoanza kusiwe na tatizo tena.

Omog alisema: “Malika si mchezaji mgeni kwangu, namfahamu, nilikuwa naye Azam kipindi cha nyuma bado nimepata sifa zake kuwa ni mzuri, lakini kwanza nataka kumwona, nikijiridhisha na kumtambua ni wa aina gani, ndio nitaamua cha kufanya.”

Hata hivyo, Malika ambaye aliingia Morogoro usiku wa juzi Jumatano, akiwa katika mazoezi hayo alikuwa kama mwenyeji kutokana na namna alivyojichanganya na wenzake.

Malika ameungana na wachezaji wengine wazawa wapya kwenye kikosi hicho kinachojifua Uwanja wa Highland mkoani Morogoro ambao ni Mdhamiru Yassin, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim wote kutoka Mtibwa Sugar, Hamad Juma kutoka Coastalna Jamal Mnyate kutoka Mwadui.