Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pamba Jiji yaita mashabiki, yasema haigomi kama Yanga

PAMBA Pict

Muktasari:

  • Pamba Jiji yenye maskani yake jijini Mwanza inayopambana kutoshuka daraja, itacheza dhidi ya JKT Tanzania Juni 18, 2025 saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba kisha itahitimisha ligi msimu huu kwa kuikaribisha KMC.

UONGOZI wa Pamba Jiji imeipiga kijembe Yanga kiaina kwa kusema watacheza mechi mbili za mwisho za Ligi Kuu na wala hatagoma kama vinara hao na kuamua kuwaita mashabiki wa timu wajitokeze kwa wingi katika mechi hizo ili wafanye kweli wakiwa nyumbani.

Pamba Jiji yenye maskani yake jijini Mwanza itacheza dhidi ya JKT Tanzania Juni 18, 2025 saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba kisha itahitimisha ligi msimu huu kwa kuikaribisha KMC.

Timu hiyo inapambana kusalia Ligi Kuu ambapo inakamata nafasi ya 12 ikivuna alama  30 katika michezo 28, ikishinda mechi saba, sare tisa na kupoteza 12, huku ikifunga mabao 20 na kuruhusu 32.

Kijembe hicho dhidi ya Yanga, kimetolewa leo Jumatano Juni 11, 2025 jijini Mwanza na Msemaji wa timu hiyo, Moses William kwa niaba ya mnejimenti ya klabu hiyo katika mkutano na waandishi wa habari uliolenga kuzungumzia maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya JKT Tanzania wakienda na kauli mbiu ya 'Tunamaliza Kibabe'.

Awali Yanga ilitishia kucheza Dabi ya Kariakoo dhidi ya Simba iliyopangwa kupigwa Juni 15 baada ya awali kushindwa kuchezwa Machi 8, lakini juzi imetoa msimamo mwingine wa kugomea mechi zote za Ligi Kuu zikiwamo mbili za mwisho dhidi ya TZ Prisons na Dodoma Jiji na ile fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida Black Stars zilizopangwa kupigwa kati ya Juni 18, 22 na 28.

William amesema kwa upande wao ishu ya 'Hatuchezi' haiwahusu kwa vile wanaihitaji mechi hiyo ili kutimiza azma ya kubakia Ligi Kuu, ambapo katika kuonyesha msisitizo wamepunguza viingilio vya mchezo dhidi ya JKT Tanzania na kuwa Sh500 kwa jukwaa la mzunguko (kwa wenye kadi za N-Card) huku jukwaa Kuu (VIP) ikiwa ni Sh5,000.

"Mechi inayofuata ni dhidi ya JKT Tanzania ni mechi ambayo tunaitaka na sisi tunasema mechi ipo na tutacheza, sisi kama Klabu tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo. Mechi hii ni ngumu na tunahitaji kweli kweli," amesema William na kuongeza; "Ukiangalia mazingira tuliyopo siyo mazuri tunahitaji umoja wa klabu kufanikisha ushindi, maandalizi na juhudi zinazofanywa na viongozi wetu ni kuhakikisha tunapata matokeo mazuri."

Akizungumzia viingilio hivyo, William amesema lengo ni kuwafanya mashabiki kufurika kwenye hizo na kufanikisha lengo la kupata alama sita ili kumaliza ligi kwa kishindo.

"Inawezekana ni kiingilio kidogo kwa hadhi ya mchezo na hadhi tuliyonayo lakini kwa mahitaji yetu ya matokeo siyo inshu, tunahitaji mashabiki waje waisapoti timu," amesema William na kuongeza;

"Tumetoa uhuru na kiwango hicho cha fedha ili kuwaunga mkono vijana wapambanie alama tau, litakuwa ni jambo la fedhea kwa viingilio hivi mashabiki kutojitokeza. Kwa sasa timu inaendelea kujipanga vizuri kuhakikisha inakuwa tayari kupata matokeo."

Ofisa huyo amesisitiza kwamba hawayumbishwi na kinachoendelea kwa sasa mitandaoni bali wanajiandaa na michezo yao kwani ili wabakia salama ni lazima washinde mechi hizo mbili jambo ambalo haliwapi wasiwasi kwa sababu wanaamini ubora wa timu yao, benchi la ufundi na jitihada zinazofanywa na uongozi.

"Pamba Jiji FC kama klabu na mnejimenti sisi tunajiadaa na michezo ya Ligi Kuu Bara na mchezo ujao pale CCM Kirumba dhidi ya JKT Tanzania sisi tutacheza. Tukifanikiwa kupata tunachokihitaji dhidi ya JKT basi mchezo dhidi ya KMC utakuwa wa furaha na huenda labda kusiwe na kiingilio," amesema.