Simba wafanya sapraizi, Mbrazili afurahia

WACHEZAJI wa Simba wamepania, baada ya kufanya sapraizi ya aina yake kiasi cha kumshangaza hadi kocha mkuu wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetamka kuwa hajawahi kuona kitu kama hicho.

Simba itakuwa wenyeji wa Raja Casablanca katika mechi ya pili ya Kundi C ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na tayari wachezaji wapo kambini tangu Jumatano.

Mastaa wa Simba wakiongozwa na Moses Phiri, Clatous Chama, Saido Ntibazonkiza na Pape Ousmane Sakho, walianza kupiga tizi siku chache tangu warejee kutoka Guinea ambako walipoteza kwa bao 1-0 mbele ya Horoya AC.

Lakini katika jambo lisilo la kawaida baada ya kumaliza mazoezi ya siku ya kwanza zaidi ya wachezaji 10 walienda kuomba ruhusa benchi la ufundi kila mmoja kwenda kupiga tizi binafsi ili kujiweka fiti zaidi.

Wachezaji hao wakiwemo wa kikosi cha kwanza walilishtua benchi la ufundi, kwani walikwenda kufanya mazoezi binafsi wakati wakiwa kambini, tofauti na ilivyozoeleka hufanya wanapokuwa mapumziko, ligi ikisimama au msimu kuisha.

Katika kuonyesha wanahitaji ushindi dhidi ya Raja Casablanca, wachezaji waliokwenda kufanya mazoezi binafsi kuna walioenda pembezoni mwa fukwe za bahari, gym na wengine kukimbia. Miongoni mwa wachezaji waliofanya mazoezi binafsi fukwe za bahari ni nahodha msaidizi Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Sakho, Mzamiru Yassin na Kennedy Juma na wengine.

Wachezaji walitaka kufanya mazoezi hayo mbali na yale waliyopewa asubuhi na benchi la ufundi ili kuongeza utimamu wa mwili na hali ya kushindana zaidi.

Wingi wa wachezaji kufanya mazoezi binafsi tena wakitokea kambini ilionekana kumfurahisha Robertinho na akiamini hilo ni miongoni mwa silaha muhimu.

“Imekuwa ni sapraizi kwangu. Ni nadra wachezaji kufanya mazoezi binafsi kipindi timu wakiwa kambini, imevutia na kuonyesha walivyo na kiu ya kufanya makubwa mbele ya Raja,” alisema Robertinho aliyetua Simba karibuni kutoka Vipers ya Uganda.

Wachezaji hawakuishia hapo hata juzi kuna wengine waliingia gym kufanya mazoezi ya nguvu.


KILA KITU POA

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema maandalizi ya mchezo wa kesho yanaenda vizuri na kilichobaki ni boli litembee.

Try Again aliwaomba mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Kwa Mkapa ili kuwachanganya Raja Casablanca.

“Nimepata nafasi ya kuzungumza na wachezaji kila mmoja ameonyesha namna gani ana hamu ya kuona Simba inapata ushindi kwenye huu mchezo mkubwa na kuendeleza rekodi ya kufanya vizuri nyumbani,” alisema Try Again.

“Benchi la ufundi linapambana kuhakikisha wachezaji wanapokea yale ambayo wanayahitaji.”