Simba waapa kambini

Muktasari:

  • Simba itaialika Horoya katika pambano hilo la Kundi C litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku ikihitaji ushindi ili kujihakikisha kwenda robo fainali ya michuano hiyo na benchi la ufundi ikijipanga ili kupata matokeo mazuri na kocha wa timu hiyo

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kwa mazoezi makali kujiandaa na pambano la kimataifa la Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya ya Guinea, litakalopigwa leo jijini Dar es Salaam huku mastaa wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi likiapa kwapa raha mashabiki wa klabu hiyo Kwa Mkapa.

Simba itaialika Horoya katika pambano hilo la Kundi C litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku ikihitaji ushindi ili kujihakikisha kwenda robo fainali ya michuano hiyo na benchi la ufundi ikijipanga ili kupata matokeo mazuri na kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' amesema mastaa wa timu hiyo wameutaza mchezo huo kwa jicho la kipekee na wameapa kupambana kuwapa raha mashabiki.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Robertinho alisema unautazama mchezo huo wa leo kama fainali na hawatakuwa na kisingizio chochote cha kuwaambia mashabiki kama watashindwa kushinda nyumbani ili kutinga hatua ya robo fainali.

Simba itaingia uwanjani kwenye mchezo huo, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza ugenini kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza dhidi ya Horoya na hadi sasa kundini ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi sita nyuma ya vinara, Raja Casablanca ya Morocco iliyotangulia mapema kutinga robo fainali.

Kocha Robertinho alisema alisema amekaa na wachezaji na kuzungumza nao na kuwaambia anataka kuona wakicheza kitimu zaidi hasa wakati ambao wakiwa hawana mpira ili kuhakikisha wanakuwa salama muda wote huku wakishambulia kwa hesabu.

Kocha huyo raia wa Brazil, alisema wachezaji wamemhakikisha watapambana kwani hilo ni pambano la kufa au kupona na hawatakuwa na kisingizio wakichemsha nyumbani, kwani wote wanaamini tiketi ya robo fainali ipo Kwa Mkapa kabla ya kwenda Morocco kumalizana na Raja.

"Hakuna cha kuturudisha nyuma, tutacheza kama timu kuhakikisha tunavuka makundi, hii ni nafasi yetu na wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo, tunapaswa kuitumia vizuri mbele ya mashabiki wanatuunga mkono, heshima yetu kwa wapinzani wetu ni kubwa, lakini hilo haliwezi kutuzuia kutimiza malengo ya kwenda robo," alisema Robertinho raia wa Brazili na kuongeza;

"Kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza anajua wajibu wake, niseme tu, siwezi kuacha nyuma silaha yangu wakati wa mapambano kwa asilimia kubwa mpango wa mchezo umekamilika kilichopo ni kuufanyia kazi tu."

Katika mazoezi ya Simba siku chache zilizopita, Robertinho ameonekana akikaa na mchezaji mmoja mmoja na makundi makundi kulingana na nafasi zao ili kuwajenga wachezaji wake kimbinu na saikolojia kwa mchezo huo ambao umebaba hatma yao.

Muda mwingi alionekana kuutumia kwa viungo wake wachezeshaji, Clatous Chama, Pape Sakho na Sadio Ntibazonkiza na washambuliaji, Moses Phiri na Jean Baleke wenye kibarua cha kuufungua ukuta wa Horoya ambao kwenye ligi yao ya ndani Guinea imeruhusu mabao manne tu kwenye michezo 14.