Simba vs Namungo, Shoo ya Kiufundi, Simba imeiva

REKODI mpya mbili zimeandikwa na Simba ambazo ni kuwa timu iliyotwaa mara nyingi taji la Ngao ya Jamii, lakini nyingine ni ile ya kuwa timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi mfululizo ambapo imelichukua mara nne.
Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii uliochezwa jijini Arusha juzi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, uliwawezesha kutwaa taji hilo kwa mara nyingine baada ya kulichukua katika miaka ya 2019, 2018, 2017, 2012 na 2011.
Kiwango bora cha nyota mpya wa Simba, Bernard Morrison, kilitosha kuamua matokeo ya ushindi kwa timu yake akihusika katika mabao yote mawili yaliyofungwa katika mchezo huo ambapo, moja lilifungwa kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na John Bocco ambayo ilitokana na Morrison kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari la Namungo.
Na bao la pili la Simba lilifungwa na Morrison mwenyewe katika dakika ya 60 ya kipindi cha pili cha mchezo huo akiunganisha vyema kwa mguu wake wa kulia, pasi ya Clatous Chama.
Mwanaspoti ilitazama mchezo na hapa inajaribu kuainisha masuala kadhaa yaliyojitokeza kuanzia dakika ya kwanza hadi filimbi ya kumaliza mchezo ilipopulizwa na mwamuzi, Ramadhan Kayoko kutoka Dar es Salaam.
TIMU BORA ZAIDI
Ilikuwa ni mechi iliyokutanisha timu mbili ambazo zilionyeshana uwezo ndani ya uwanja, zikicheza soka la pasi na nafasi huku wachezaji wa kila timu wakijaribu kupambana kwa ufanisi wake ili kuhakikisha timu yake inapata ushindi.
Hata hivyo, walikuwa ni Simba ambao walinufaika zaidi na utofauti mkubwa wa uwezo wa mchezaji mmoja mmoja waliokuwa nao dhidi ya Namungo.
Ufundi na ubunifu wa idadi kubwa ya wachezaji wa Simba katika kuvunja mbinu na mikakati ya Namungo FC, ulizaa matunda kwa kuwalazimisha wapinzani wao kufanya makosa ya mara kwa mara ambayo yaliwafanya waibuke na ushindi huo.
Ubora wa wachezaji wengi wa Simba ulisababisha juhudi za nyota wachache wa Namungo FC kama vile Lucas Kikoti, Nourdine Barola na Nzigamasabo Styve zisiwe na faida yoyote kwa upande wa timu yao.
SIMBA ILIPOISHIA
Kati ya wachezaji 11 walioanza kwenye kikosi cha kwanza, wapya walikuwa ni wawili tu ambao ni beki wa kati, Joash Onyango na winga Bernard Morrison na wengine tisa ni wale waliokuwemo msimu uliopita.
Upangaji huo wa kikosi ulionekana kuwa na mchango chanya kwa Simba kwani wachezaji wake walionyesha uelewano mkubwa na hiyo iliwatengenezea mazingira rahisi hata wapya wawili kuendana haraka na staili ya uchezaji ya timu.
Ni tofauti na Namungo FC ambayo mara kadhaa ilionekana kukosa muunganiko kutokana na kuwa kundi kubwa la wachezaji wapya walioanza kikosini.
Katika kikosi kilichoanza cha Namungo, wachezaji waliokuwemo msimu uliopita walikuwa ni sita ambao ni Barola, Steven Duah, Hamis Fakhi, Abeid Athuman, Lucas Kikoti na Nzigamasabo Styve.
WAAMUZI SAFI
Ubora na ushindani ulioonyeshwa na timu hizo mbili kwenye mechi hiyo hapana shaka ulichagizwa na kazi nzuri iliyofanywa na marefa sita waliochezesha mechi hiyo ambao ni Ramadhan Kayoko, Mohamed Mkono, Frank Komba, Ahmed Arajiga, Abubakar Mturo na Abdallah Mwinyimkuu.
Waamuzi hao walisimama katika nafasi sahihi muda wote, waliona vyema matukio na kuchukua uamuzi kwa haraka na waliwasiliana vyema.
NAMUNGO TUIWEKEE AKIBA
Kikosi cha Namungo FC kimeongezewa sura 10 mpya ambazo ni Stephen Sey, Abdulhalim Humoud, Amani Kyata, Shiza Kichuya, Jafari Mohamed, Sixtus Sabilo, Fred Tangalu, Frank Magingi, Iddi Kipagwile na Haruna Shamte.
Katika mchezo wa juzi dhidi ya Simba, baadhi yao wameonyesha uwezo wa juu katika mechi chache walizoichezea timu hiyo na kuna wengine hawajaweza kuonyesha kiwango cha kuvutia.
Inawezekana hilo limetokana na mahitaji ya timu hizo katika mchezo wa juzi lakini pindi ligi itakapoanza, hakutokuwa na utetezi tena.
ONYANGO, SEY BALAA
Usajili wa beki Joash Onyango ambao Simba waliufanya, ulibezwa na baadhi ya watu wakidai kuwa mlinzi huyo wa kati kutoka Gor Mahia, hana uwezo mkubwa wa kuisaidia Simba kupata matokeo.
Ni kama ilivyokuwa kwa Namungo ambayo baadhi ya watu walishangazwa na usajili wa straika Stephen Sey kutoka Singida United.
Hata hivyo, kiwango kilichoonyeshwa na wawili hao kinaweza kubadili hisia na mitazamo ya wale waliowabeza.
Sey ameonekana kuwa mwiba kwa walinzi wa timu pinzani kutokana na kasi, uwezo wa kunusa hatari na kusimama katika nafasi sahihi pamoja na kumiliki mpira.
Kwa Onyango, beki huyo wa kati ameonekana kuwa mahiri katika kupora mipira kwa washambuliaji wa timu pinzani, kutibua mashambulizi na kuwasiliana vyema na walinzi wenzake.
MAKOCHA WAKOSHWA
Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck aliipongeza timu yake kwa kucheza vizuri.
“Tulicheza vizuri na kila mmoja alitimiza wajibu wake katika kukaba na kushambulia. Halikuwa suala la mchezaji mmoja mmoja bali wajibu wa kitimu.
“Timu ilionesha muunganiko mzuri na naamini tukiendelea hivi tutafanya vizuri zaidi katika msimu mpya,” alisema Vandenbroeck
Kocha wa Namungo FC, Hitimana Thiery alisema kuwakosa baadhi ya wachezaji wake kumewagharimu.
“Hatukuwa na Carlos Protas na pia Edward Manyama hivyo kukosekana kwao kulitupa ugumu. “Sisemi kwamba waliocheza walifanya vibaya bali wangekuwepo hao tungekuwa imara zaidi.
Hata hivyo, mwisho wa siku mechi imemalizika na nawapongeza Simba kwa ushindi. Kwa upande wetu tunakwenda kufanya marekebisho ya mapungufu tuliyokuwa nayo,” alisema Thiery.