Simba Sh240 mil, Yanga 540 mil

KUAHIRISHWA kwa mechi ya watani juzi jioni kumewapa hasara wachezaji Simba na Yanga.

Simba wamepoteza zaidi ya Sh.240 milioni huku Yanga ikikosa Sh. 540milioni.

Kwa mujibu wa habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni wachezaji wangepata kiwango hicho kama wangeshinda mechi hiyo.

Mchezo huo uliahirishwa baada ya Yanga kugomea kucheza saa 1 usiku kutoka muda wa saa 11 uliokuwa umetangazwa awali na Mamlaka za soka.

Mmoja wa wachezaji wa Simba aliidokeza Mwanaspoti uongozi ulipiga nao msosi siku moja kabla ya gemu na kuwaahidi mkwanja huo na ulikuwa uongezeke zaidi.

“Jambo lingine tulitamani kushinda mechi hiyo ili kuturahisishia safari yetu ya mbio za ubingwa kwani hayo ndio malengo tuliyonayo msimu huu,” alisema mchezaji huyo ambaye ni tegemeo kwenye kikosi cha kwanza.

Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alisema mechi haijachezwa kwa maana hiyo ile ahadi ya pesa waliyopanga kuwapa wachezaji wao kama wangeshinda maana yake hakuna.

“Tunajipanga katika mchezo mwingine, siku nyingine ambayo itapangwa ndio tutafahamu tutaweka ahadi kama hii au tutaongeza,” alisema.


YANGA SH 540

Yanga wamewapa mapumziko ya siku moja mastaa wao lakini wanagugumia maumivu ya kupoteza Sh540 milioni.

Yanga waliahidiwa na matajiri wao jumla ya Sh540 milioni kiliandaliwa kwa kupewa wachezaji endapo wangeshinda mchezo huo.

Katika mgawanyo huo kila mchezaji ambaye angekuwa uwanjani yaani wale 11 na wengine saba wanaokaa katika benchi basi wangejihakikishia Sh30 milioni kila mmoja.

Mzigo huo unafanya kwa wachezaji hao 18 kiasi hicho cha Sh540 kilikuwa tayari kinawasubiri lakini hata hivyo mchezo huo kuahirishwa huku wao wakigomea kucheza kwa saa 1:00 usiku wakitaka muda wa awali saa 11:00 jioni kulipoteza ahadi hiyo.

Kiasi hicho ni mara mbili katika ahadi ambayo wachezaji wa Simba walipewa na mabosi wao wakiahidiwa kupewa kaisi cha Dola 100,000 (zaidi ya Sh 231). Mamlaka za soka nchini zinapanga upya tarehe ya mchezo huo.