Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba sasa uhakika

Muktasari:

  • Mpaka sasa tayari Simba imewasainisha mabeki Emmanuel Semwanza, Malika Ndeule, kiungo Mdhamiru Yassin na winga Jamal Mnyate pamoja na straika Blagon Frederick aliyewahi kuichezea Asante Kotoko ya Ghana.

SIMBA inafanya mambo yake kimya kimya na tayari imekamilisha usajili wa nyota wanne wa ndani na mmoja wa kigeni ambao Mwanaspoti imebaini kuwa nyota hao watakipangua kabisa kikosi cha timu hiyo msimu ujao.

Mpaka sasa tayari Simba imewasainisha mabeki Emmanuel Semwanza, Malika Ndeule, kiungo Mdhamiru Yassin na winga Jamal Mnyate pamoja na straika Blagon Frederick aliyewahi kuichezea Asante Kotoko ya Ghana.

Licha ya Rais wa Simba, Evans Aveva kuliambia Mwanaspoti wiki iliyopita kuwa wamepanga kusajili nyota 10 wapya, imebainika kuwa nyota watano wa sasa wanapewa nafasi kubwa ya kukibadili kikosi hicho ambacho kitakuwa na kazi kubwa ya kuwania taji la Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kulikosa kwa misimu minne mfululizo.

Mabeki, Ndeule na Semwanza wanajipanga kuchukua nafasi za Hassan Isihaka aliyekalia kuti kavu na Emiry Nimubona ambaye tayari Simba imemalizana naye na amerejea kwao Burundi.

Mabeki hao wawili wataongeza nguvu katika safu hiyo ya ulinzi sambamba na Novatus Lufunga ambaye ana uhakika wa kubaki pamoja na Juuko Murshid ambaye mpaka sasa dili lake la kwenda Lebanon bado lipo njiapanda.

Kiungo Mdhamiru Yassin anapigiwa upatu wa kuifumua safu ya kiungo ya Simba hasa kuchukua nafasi ya Said Ndemla aliyeshuka kiwango pamoja na Mwinyi Kazimoto ambaye mara nyingi amekuwa akikosa ubunifu na kushindwa kutoa pasi za mabao licha ya kuwekewa viungo wawili nyuma Justice Majabvi na Jonas Mkude.

Mnyate anapata nafasi ya moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kuchukua nafasi ya Brian Majwega aliyeachwa pamoja na Peter Mwalyanzi ambaye mpaka sasa yupo katika orodha ya wachezaji ambao wamekalia kuti kavu.

Simba imemsajili Mnyate kutokana na uwezo wake mkubwa wa kupiga krosi kutokea upande wa kulia ili kuifanya timu yao iwe na uwiano mzuri badala ya kutegemea tu krosi za upande mmoja kutoka kwa Mohammed Hussein ‘Zimbwe Jr’.

Straika huyo Muivory Coast ambaye aliletwa Simba na kipa wao Vincent Angban atachukua nafasi ya Raphael Kiongera ambaye ameachwa huku akitarajiwa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kama straika namba moja ama kucheza sambamba na Hamis Kiiza ambaye mpaka sasa Simba bado haijakamilisha taratibu za kuachana naye licha ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe kudai kuwa hawana mipango naye.

Nahodha wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema mabadiliko yanayofanyika Msimbazi kwa sasa yanazingatia vigezo vyote kwani kwa sasa lengo la timu ni kuhakikisha kuwa msimu ujao wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu.

“Naamini kila kinachofanyika sasa kinazingatia ripoti ya benchi la ufundi, kila mmoja aliona timu inahitaji mabadiliko na ndicho wanachofanya sasa kuhakikisha mabadiliko yanakuwepo,” alisema Mgosi.

“Iwe ni wachezaji wawili ama kumi wapya lakini ukweli ni kwamba yote hayo yanafanyika ili kujenga timu imara, msimu ujao hatutaki kuwa na sababu kwanini tumeukosa Ubingwa,” aliongeza.

KAVUMBAGU ATAJWA

Katika hatua nyingine, beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa amewataka mabosi wa timu yake hiyo ya zamani waache kuhaha kusaka wachezaji nje ya nchi kwani kuna wachezaji wengi wazuri hapa nchini ambao wanaweza kuwasaidia.

Pawasa aliwataja Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar na Didier Kavumbagu wa Azam kuwa miongoni mwa nyota ambao wanaweza kucheza Simba kwa mafanikio na kuwataka mabosi wa timu hiyo kufanya kweli.

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwanaspoti au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz

Beki huyo wa zamani wa Taifa Stars alisema Mbonde ana uzoefu mkubwa Ligi Kuu na amewahi hadi kucheza timu ya taifa wakati Kavumbagu ni miongoni mwa mastraika wapambanaji ambao hawatumiki vizuri kwa sasa.

“Hakuna haja ya Simba kwenda kuhaha nje ya nchi kusaka wachezaji kwani hapa nchini kuna wachezaji wazuri tu wa kuwasaidia,” alisema Pawasa.

“Mfano mchezaji kama Mbonde (Salim) ni beki mzuri na amewahi hadi kuonyesha uwezo kwenye timu ya taifa, au Kavumbagu (Didier) ambaye ni mpambanaji lakini amekuwa hapati nafasi pale Azam, huyu anaweza kuisaidia Simba,” alisema.