Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba rasmi Ligi ya Mabingwa, Ahoua akipiga hat trick

SIMBA SC Pict
SIMBA SC Pict

Muktasari:

  • Simba imefikisha pointi hizo baada ya kuifunga Pamba Jiji mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika leo Alhamisi Mei 8, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

RASMI Simba SC ina tiketi ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao 2025-2026, hiyo ni baada ya kufikisha pointi 66 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ambazo haziwezi kufikiwa na timu zilizopo chini yake.

Simba imefikisha pointi hizo baada ya kuifunga Pamba Jiji mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika leo Alhamisi Mei 8, 2025 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Jean Charles Ahoua kwa kiasi kikubwa ndiye aliyeimaliza kazi hiyo baada ya kufunga mabao matatu dakika ya 16, 37 na 52 ambapo mawili yalitokana na mipira ya kutenga.

Bao la kwanza Ahoua alifunga kwa penalti baada ya Joshua Mutale kufanyiwa faulo eneo la hatari na winga Zabona Mayombya.

Kuingia kwa bao hilo, kuliifanya Pamba Jiji kupambania pointi ikifanya mashambulizi kadhaa kupitia mshambuliaji, Mathew Tegis, lakini safu ya ulinzi ya Simba chini ya kipa Moussa Camara ilikaa imara.

Katika harakati za kuongeza mabao, dakika ya 37 Simba iliendeleza mashambulizi, ambapo Mutale alifanyiwa faulo nje kidogo ya eneo la hatari la Pamba Jiji ndipo Ahoua akaitumia vizuri nafasi hiyo kufunga moja kwa moja na kumuacha kipa Mohamed Kamara akishindwa kuruka.

Kipindi cha kwanza kilichokuwa na mashambulizi kadhaa pande zote huku faulo za hapa na pale zikimfanya mwamuzi wa kati, Shomari Lawi kuonyesha kadi tatu za njano kwa wachezaji wawili wa Pamba Jiji na moja Simba, kilimalizika kwa Simba kuwa mbele kwa mabao 2-0.

Mwanzoni mwa kipindi cha pili, Pamba Jiji ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Paulini Kasindi na kuingia Saleh Masoud, huku Simba ikimtoa Abdulrazack Hamza na kuingia Che Fondoh Malone.

Dakika ya 52, Ahoua alihitimisha hat trick akiunganisha kwa kichwa krosi ya Ellie Mpanzu ambaye hii ni asisti yake ya tatu kwenye ligi msimu huu.

Baada ya Simba kufunga bao hilo, Pamba Jiji ilionekana kasi ya mashambulizi kupungua hali iliyotafsiriwa kukata tamaa.

Dakika ya 60, Simba ilifanya mabadiliko mengine ya wachezaji watatu, Shomari Kapombe alimpisha Kibu Denis, Valentine Nouma aliingia kuchukua nafasi ya Jean Charles Ahoua na Fabrice Ngoma akampisha Debora Mavambo.

Dakika 72, Kocha wa Pamba Jiji, Fred Felix 'Minziro' alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu ambapo Shassir Nahimana alimpisha Samson Madeleke, Zabona Mayombya kampisha Hamadi Majimemgi na Kenneth Kunambi kampisha Deus Kaseke. Dakika ya 82, Ibrahim Abraham alimpisha Cherif Ibrahim.

Pia Kocha wa Simba, Fadlu Davids, dakika ya 75 alimtoa Joshua Mutale na kuingia Ladack Chasambi.

Wakati mchezo ukielekea ukingoni, dakika ya 83 na 85, Leonel Ateba alifunga bao la nne na la tano ambapo sasa amefikisha 12.

Mathew Tegis aliifungia Pamba Jiji bao pekee dakika ya 88 na kuifanya timu hiyo kuwa na mwendelezo wa kufunga mechi tano mfululizo.

AHOUA AREJESHA UFALME WAKE
Mabao hayo matatu yamemfanya Ahoua kurejesha ufalme wake wa kukaa kileleni kwenye chati ya wafungaji baada ya kufikisha 15, akimzidi Clement Mzize wa Yanga mwenye 13.
Kabla ya mchezo huu, Ahoua alikuwa na mabao 12 ambayo awali yalimuweka kileleni kabla ya kuzidiwa na Mzize wakati Simba ikiwa na majukumu mechi za kimataifa.

Mbali na hilo, Ahoua msimu huu ameonekana kuwa mkali wa kufunga penalti kwani katika sita alizopiga zote zimetinga nyavuni.

Simba ikiwa ndiyo timu iliyofaidika na mikwaju mingi ya penalti kwenye ligi msimu huu ambayo ni 13, Ahoua amefunga sita sawa na Leonel Ateba ambaye yeye amepiga saba na kukosa moja.

CAMARA ATIBULIWA
Kipa wa Simba, Moussa Camara ametibuliwa kumaliza na clean sheet baada ya kuruhusu bao dakika za mwisho ambapo sasa zimebaki 16 katika mechi 23 alizocheza sawa na dakika 2070.

Kwa kufikisha clean sheet hizo, Camara anahitaji tatu katika mechi tano zilizobaki ili kufikisha 19 ambazo hazitafikiwa na kipa yeyote msimu huu na kumfanya kuweka ufalme wake msimu wa kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara.

Kwa sasa, Camara mwenye clean sheet 16, amemzidi mbili Djigui Diarra wa Yanga aliyecheza mechi 20 na kutoka uwanjani mara 14 bila kuruhusu bao. Katika mechi nne zilizobaki kwa Yanga, Diarra akicheza zote bila ya kuruhusu bao atafikisha clean sheet 18.