Simba noma Dar mpaka mkoa

Simba squad
Muktasari:
Simba sasa imefikisha pointi 42 sawa na Azam ambayo ilipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Mwadui Shinyanga katika pambano jingine lililiochezwa jana, Dar es Salaam.
HII sasa sifa. Licha ya kupunguzwa dozi zake, lakini Simba jana Jumapili iliendeleza wimbi la ushindi ikishinda mechi ya sita mfululizo tangu iwe chini ya Kocha Jackson Mayanja, baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0. Yaani wao wanapiga kotekote kuanzia Dar mpaka mkoani waoa wangonga tu kinomanoma.
Simba ikiwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ilipata ushindi huo, huku nyota wake Ibrahim Ajib akipoteza penalti. Ajib alishindwa kufunga penalti hiyo iliyotolewa kitatanishi na mwamuzi Mathew Akrama dakika ya 82, baada ya kuangushwa, lakini shuti lake lilidakwa na kipa, Andrew Ntala.
Simba sasa imefikisha pointi 42 sawa na Azam ambayo ilipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Mwadui Shinyanga katika pambano jingine lililiochezwa jana, Dar es Salaam.
Simba iliandika bao sekunde chache kabla ya mapumziko kupitia kwa Ajib aliyemaliza krosi murua ya Hamis Kiiza. Kipindi cha kwanza, Simba ilipoteza nafasi nyingi kulinganisha na wenyeji walioshambulia kwa kushtukiza.
Baada ya kumtoa Haji Ugando na kumuingiza Danny Lyanga na kisha kumtoa Kiiza na kumuingiza Brian Majwega, Simba ilicharuka zaidi hadi kuifanya Kagera ibadili wachezaji watatu kwa mpigo ikiwatoa Adam Kingwande, George Kavila na Martin Lupati na kuwaingiza Idd Kurachi, Babu Ali na Ramadhani Kiparamoto.
Kagera ilimaliza mchezo pungufu baada ya beki wao.Daud Jumanne kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi dakika za lala salama kwa madai ya kumtolea lugha chafu. Baada ya kipyenga cha mwisho waamuzi wa mchezo huo walitolewa chini ya ulinzi wa polisi kutokana na mashabiki kutaka kuwanyoosha wakiamini waliibeba Simba. Simba itaendelea kubaki mjini hapa kwa ajili ya mechi ijayo na Stand United kabla ya kuivaa Yanga Februari 20.
YANGA
YAIFANYIZIA JKT
Ikiwa na hasira ya kupoteza pointi tano ugenini katika mechi mbili zilizopita, Yanga iliifanyia kweli JKT Ruvu kwa kuichapa 4-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ilipoteza mchezo wa kwanza ugenini katika duru la pili dhidi ya Coastal Union kabla ya kulazimishwa sare ya 2-2, ilishuka Uwanja wa Taifa ikiwa na hasira.
Simon Msuva na Issofou Boubacar ‘Diego’ itabidi wajilaumu kwa kupoteza nafasi nyingi za kufunga hasa kipindi cha kwanza licha ya kila mmoja kufunga.
Msuva aliandika bao dakika ya 12 kabla ya Diego kuongeza la pili dakika chache kabla ya mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa kashkash na kosa kosa nyingi kwa timu zote kabla ya Yanga kuwatoa Malimi Busungu na Diego na kuwaingia Paul Nonga na Deus Kaseka, huku Ruvu ikiwatoa Gaudence Mwaikimba na Paul Mhidze na kuwaingia Abdulrahman Mussa na Hamis Shango mabadiliko yaliyoisaidia Yanga baada ya kupata bao la tatu lililofungwa kwa kichwa na Donald Ngoma dakika ya 63, likiwa bao lake la 10 katika msimu wake wa kwanza Ligi Kuu.
Dakika za majeruhi Msuva aliiandika Yanga bao la nne na kufikisha mabao sita katika ligi ya msimu huu.
Yanga imejiimarisha kileleni ikiwa na pointi 43 ikifuatiwa na Simba kisha Azam ambayo imerejea kwenye ligi baada ya kuwa Zambia kwenye michuano maalum na kuibuka vinara.
Azam ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui, bao lililofungwa na Kipre Tchetche dakika ya 18. Azam ina michezo miwili mkononi za viporo.
Katika mechi nyingine za ligi Mtibwa Sugar iliazimishwa sare ya 1-1 na Ndanda huku Majimaji ikiiduwaza Mgambo kwa kuichapa bao 1-0, wakati Toto Africans iliichapa Coastal 2-1 jijini Mwanza na Mbeya City na Prisons zikitoka sare ya 0-0.
Imeandikwa na Mwanahiba Richard, Shinyanga, Geofrey Kahango, Mbeya na Khatimu Naheka na Gift Macha, Dar es Salaam.