Simba: Njooni mhesabu

SIMBA inashuka uwanjani jioni ya leo kuikabili Nyasa Big Bullets ya Malawi katika mchezo wa marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha wa mpito, Juma Mgunda akiwatoa hofu mashabiki kwa kuwaambia ‘hatutarudia tena makosa’ na kuwaita wajitokeze Kwa Mkapa kupata burudani.

Simba na Bullets zitavaana kuanzia saa 10 jioni ikiwa na hazina ya ushindi wa mabao 2-0 iliyopata ugenini, huku mashabiki wakiwa na kumbukumbu ya mechi ya msimu uliopita iliposhinda pia 2-0 dhidi ya Jwaneg Galaxy ya Botswana ugenini, lakini ikaja kupasuka nyumbani kwa mabao 3-1 na kutolewa.

Kocha Mgunda alisema wanaingia uwanjani leo kwa tahadhari zote kuhakikisha kilichojitokeza mbele ya Jwaneng hakijirudii, huku akiwaita mashabiki Kwa Mkapa kwenda kupata burudani kwani nia yao ni kusonga mbele michuano hiyo ya CAF.

“Binadamu anajifunza kutokana na makosa. Kuna makosa yalifanyika yakasababisha ushindi ule tukiwa ugenini ikashindwa kuulinda hapa. Lakini ngoja niwaambie tu, mechi inaisha hadi filimbi ya mwisho ikilia Ile mechi ya mwanzo ya Malawi ilikuwa kama kipindi cha kwanza,” alisema Mgunda.

“Tunalijua hilo na tunalifahamu. Wachezaji wanalitambua hilo na wako tayari kupambana tukiamini kwa uwezo wa Mungu kilichotokea nyuma hakijirudii tena,” alisema Mgunda, huku nahodha msaidizi, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alisema wachezaji wamejiandaa kisaikolojia kuhakikisha kazi waliyoifanya Malawi wanaimalizia leo.

“Wachezaji tumehamasishana na tumeelekezana hii ni mechi muhimu ambayo tunatakiwa kufanya vizuri nyumbani. Katika mechi ya kwanza Malawi tulihamasishana kuhakikisha tunapata ushindi na baada ya hapo tukaambiana tuna mechi ya pili nyumbani na ukizingatia kilichotokea mwaka jana, hatutaki kuruhusu kitokee tena,” alisema Tshabalala.

Akizungumzia kikosi, Mgunda alisema; “Wachezaji wote wako vizuri na tayari kuhakikisha atakayepewa gwanda la Simba kesho (leo) naamini atawaiwakilisha vizuri Simba.”

Bila ya shaka Simba itaingia katika mchezo wa leo ikitegemea zaidi makali ya safu yake ya ushambuliaji ambayo imefunga bao katika kila mechi ya mashindano msimu huu ambapo imepachika jumla ya mabao 11 katika michezo sita.

Urejeo wa Sadio Kanoute unaweza kuifanya Simba ianze kwa mfumo wa 4-2-3-1 ambapo kiungo huyo wa Mali anaweza kucheza sambamba na Jonas Mkude katika jukumu la kuilinda safu yao ya ulinzi, huku juu wakitarajiwa kuwepo Clatous Chama, Pape Sakho na Augustine Okrah wakati Moses Phiri atasimama kama mshambuliaji wa kati.

Safu ya ulinzi bila shaka itakuwa na Aishi Manula langoni, mabeki wa pembezi ni Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na beki ya kati itakuwa na Henock Inonga na mmoja kati ya Joash Onyango ama Mohamed Ouattara.

Waamuzi wa pambano hilo ni Mahmood Ali Ismail akisaidiwa na Ibrahim Mohamed na Omer Hamid Mohamed watakaokuwa refa msaidizi namba moja na refa msaidizi namba mbili huku mwamuzi wa akiba akiwa ni Abdalaziz Yasir wote wakiwa ni Wasudan.

Takwimu zinaonyesha Simba imekuwa ikifanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ikiwa nyumbani, kwani katika mechi 10 zilizopita za CAF, imeibuka na ushindi mara tisa na kupoteza mara moja tu, huku ikifunga mabao 24 sawa na wastani wa mabao 2.4 na kufungwa matano ni wastani wa bao 0.5 kwa mchezo pia rekodi zinaonyesha katika mechi hizo zote zilizopita Simba imefunga bao.