Simba, Mwadui nguvu sawa dakika 45, Mwanamke atinga uwanjani

Muktasari:
- Simba licha ya kucheza kwa kujiamini, lakini Mwadui walitulia na kucheza kwa nidhamu kubwa na kuweza kwenda mapumziko kwa suluhu ya bila kufungana.
Shinyanga. Licha kwenda mapumziko kwa nguvu sawa lakini Simba itajilaumu kwa kukosa nafasi tatu ambazo zingeweza kuwapeleka kifua mbele dakika 45 za awali.
Simba ilionekana kuwazidi wapinzani lakini Mwadui walicheza kwa nidhamu kubwa huku wakiwa makini kuondosha hatari zilizokuwa zikilenga lango lao.

Awali ilikuwa dakika ya pili Clatous Chama alipoukokota mpira na kufanikiwa kuwapenya mabeki na kubaki na pekeake lakini shuti lake liliishia mikononi mwa Kipa Mussa Mbise.

Kama haitoshi, Chama tena dakika ya 35 alikosa nafasi ya wazi baada ya pasi yake kuokolewa na Mbise kabla ya Raly Bwalya naye shuti lake kugonga nguzo na kurudi uwanjani.

Mwadui ambao walionekana kutulia muda wote walipambana na kupata nafasi moja ambayo Straika wake, Mohamed Hashim ambaye alimkunja chenga Wawa na shuti lake kupaa nje ya lango ikiwa ni dakika ya 4
Mwanamke atinga uwanjani
Wakati mprira ukiendelea, mwanamke mmoja amezua mshangao kwa wadau na mashabiki wa soka baada ya kuvamia uwanjani na kudakwa na polisi.
Tukio hilo limetokea wakati wa mchezo ukiendelea ambapo polisi walikuwa makini kumnasa shabiki huyo haraka na kumpeleka nje ya uwanja.
Ilikuwa ni dakika ya 33 ambapo shabiki huyo akitokea upande wa Magharibi ya uwanja walipokuwa polisi na viongozi wa Simba na kutinga uwanjani.
Mashabiki waliokuwa wakifuatilia kandanda walibaki na bumbuwazi wakijiuliza alikotokea na sababu iliyomfanya anavamia dimbani bila woga.
Mwanaspoti ambalo linafuatilia matukio yote uwanjani hapo lilimshuhudia shabiki huyo akinyanyuliwa mzimamzima na polisi na kuondoshwa eneo hilo hadi nje ya uwanja.