Simba, Mtibwa lawama njenje

Muktasari:

  • Simba ambao ni wenyeji wa mechi hiyo wapo nafasi ya tatu kwenye msimo wa ligi na alama 47 baada ya mechi 22 huku Mtibwa ikiwa mkiani mwa msimamo na alama 17 huku timu zote zikitafuta ushindi ambao ni muhimu zaidi kwa kila upande na timu itakayopoteza basi itakuwa imepoteza matumaini ya mipango yao kwa sasa.

Baada ya dakika 90 za mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Mtibwa Sugar itakayopigwa kesho Mei 3, 2024 kuanzia saa 10:00 jioni Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam lawama litakuwa jambo linalofuata kwa moja ya timu hizo au zote kwa pamoja.

Simba ambao ni wenyeji wa mechi hiyo wapo nafasi ya tatu kwenye msimo wa ligi na alama 47 baada ya mechi 22 huku Mtibwa ikiwa mkiani mwa msimamo na alama 17 huku timu zote zikitafuta ushindi ambao ni muhimu zaidi kwa kila upande na timu itakayopoteza basi itakuwa imepoteza matumaini ya mipango yao kwa sasa.

Wekundu wa Msimbazi tayari wamekata tamaa ya kutwaa ubingwa msimu huu na sasa wanawania nafasi ya pili ili kupata nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Hata hivyo wakali hao wa Msimbazi wanakabiliana na ushindani mkubwa katika nafasi hiyo na Azam iliyokaa katika nafasi hiyo na alama 54 baada ya mechi 24.

Mchezo huu ni wa muhimu zaidi kwa Simba kwani utaipa matumaini ya kumaliza nafasi ya pili kwani inatakiwa kushinda mechi zote nane zilizobaki ili kumaliza ligi ikiwa katika eneo hilo. Mechi hizo nane ni pamoja na hiyo ya kesho lakini pia ile itakapokutana na mshindani wake katika nafasi hiyo, Azam. Kama Simba itashinda mechi hizo zote basi itakuwa na uhakika wa kumaliza na alama 71 zitakazoiweka nafasi ya pili lakini kama itashindwa kufanya hivyo basi itakuwa imejiweka mtegoni.

Ikumbukwe Simba imeshiriki Ligi ya Mabingwa kwa misimu sita iliyopita mfululizo hivyo ikishindwa kufuzu kwa msimu ujao itakuwa ni rekodi mbaya kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu mara 22.

Kwa upande wa Mtibwa ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu mara mbili wakichukua kombe hilo mwaka 1999 na 2000, wanahitaji alama tatu katika mchezo huo ili kurejesha matumaini ya kutoshuka daraja moja kwa moja.

Mtibwa yenye alama 17 baada ya mechi 23 ikiwa mkiani mwa ligi, inahitaji kushinda mechi zake saba zilizobaki ili kuwa na uhakika wa kubaki Ligi Kuu.

Kama itashinda mechi hizo saba ikiwemo ya kesho dhidi ya Simba itafikisha alama 38 ambazo kwa sasa ni timu nne pekee zimevuka hapo ambazo ni Simba, Azam na Yanga inayoongoza ligi na pointi 62.

Endapo Mtibwa itapoteza mechi hiyo basi huenda ikawa inaendelea kujichimbia kaburi na kuiaga Ligi Kuu mdogo mdogo.

Aidha mchezo huo utakuwa wa kila timu kutafuta ushindi baada ya kuukosa katika mechi tano zilizopita mfululizo.

Kila timu katika mechi zake tano zilizopita haijashinda hata moja ambapo zote zimepoteza mara tano na kutoa sare mara mbili, hivyo leo Simba na Mtibwa zitakuwa zikitafuta ushindi baada ya ukame wa mechi tano bila alama tatu.

Hata hivyo rekodi zinaibeba zaidi Simba pale inapokutana na Mtibwa kwani katika mechi tano za mwisho zilizokutanisha timu hizo, Wekundu wa Msimbazi wameibuka na ushindi mara nne na kutoa sare moja.

Simba itakosa huduma ya kiungo wake Clatous Chama aliyefungiwa mechi tatu baada ya kumkanyaga kwa makusudi beki wa Yanga Nickson Kibabage pale timu zao zilipokutana lakini pia huenda ikawakosa wachezaji wake muhimu, Saidi Ntibazonkiza, Henock Inonga, Shomari Kapombe na Kibu Denis kutokana na majeraha. Kwa upande wa Mtibwa itakuwa na kikosi chake kamili kikiongozwa na nahodha Oscar Masai.

Eneo la mabeki na makipa kwa timu zote mbili ndilo linaonekana kuwa na shida zaidi. Kwa Simba ambayo mara kwa mara eneo hilo hucheza Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Henock Inonga na Che Malone Fondoh limeruhusu mabao 23 katika mechi 22 ilizocheza ikiwa ni zaidi ya wastani wa bao moja kwenye kila mchezo huku kwa Mtibwa wanapocheza mara kwa mara, Ndikumana Justine, Nickson Kasami, Jimmyson Mwanuke, Masai na Nasri Kombo limeruhusu mabao 39 ikiwa ni zaidi ya wastani wa bao moja kwa kila mechi.

Bato kubwa katika mchezo huo itakuwa eneo la kiungo ambapo kwa Simba wanaocheza mara kwa mara ni Babacar Sarr, Fabrice Ngoma na Sadio Kanoute huku kwa Mtibwa wakikipiga Juma Nyangi, Nassoro Kapama na Abdul Hilal ambapo ndio chanzo cha mashambulizi ya kila timu.

Eneo lingine lenye nafasi ya kuamua mechi hiyo ni kwenye mabenchi ya ufundi ambapo Mtibwa inaongozwa na Zuberi Katwila huku Simba ikiwa chini ya Juma Mgunda anayekaimu nafasi ya kocha mkuu baada ya Abdelhak Benchikha kuondoka.

Makocha hao wa timu zote mbili wamekuwa na utamaduni wa kubadili wachezaji na mifumo kutokana na aina ya mechi jambo ambalo kwa atakayechanga vyema karata zake atakuwa na mechi bora.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Katwila alikiri mchezo utakuwa mgumu lakini wanahitaji ushindi zaidi ili kurejesha matumaini.

"Ni mchezo mgumu lakini tunachohitaji ni ushindi na kila mmoja analijua hilo. Tumejipanga na soka ni mchezo wa dakika 90 baada ya muda huo tutajua nini kimetokea," alisema Katwila aliyewahi kuichezea timu hiyo.

Kocha wa Simba, Mgunda alieleza kukiandaa vyema kikosi chake na kuwa tayari kwa mchezo ambao ameahidi timu yake itatoa burudani.

"Tumejiandaa vyema na tupo tayari kwa mchezo, nawaomba Wanasimba wajitokeze kwa wingi uwanjani kuja kupata burudani," alisema Mgunda ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa soka nchini.

Beki wa zamani wa Simba, Nassoro Cholo alisema mechi na Mtibwa huwa ngumu lakini mara nyingi Simba inashinda kutokana na uzoefu.

"Simba na Mtibwa huwa na ushindani lakini mara nyingi Simba hushinda kutokana na ubora na uzoefu wa kutosha kuwashinda Mtibwa lakini hawapaswi kuishi katika rekodi hizo bali wachezaji wapambane kuhakikisha timu inashinda," alisema Cholo aliye visiwani Zanzibar akifanya shuguli za uvuvi baada ya kustaafu soka.

Mshambuliaji wa zamani wa Mtibwa na Simba, Mussa Mgosi alisema kila timu ina nafasi ya kushinda mechi hiyo kutokana na uhitaji zaidi wa matokeo uliopo.

"Timu zote zinataka ushindi lakini matokeo ya soka huwa hayatabiriki. Nadhani watakaojipanga vyema ndio watashinda," alisema Mgosi ambaye kwa sasa ni Kocha wa Simba Queens.