Azania yaanza vyema TCA Inter-Academy

Muktasari:
- Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa UDSM, Azania ndiyo walioanza kubeti na walitengeneza mikimbio 149 baada ya kumaliza mizunguko yote 30 wakiwa wamepoteza wiketi 9.
AZANIA Boys imeanza vyema ligi ya TCA Inter-Academy baada ya kuifunga Tanga Boys kwa mikimbio 69 katika mchezo wa kriketi ya mizunguko 30 iliyochezwa jijini mwishoni mwa juma.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa UDSM, Azania ndiyo walioanza kubeti na walitengeneza mikimbio 149 baada ya kumaliza mizunguko yote 30 wakiwa wamepoteza wiketi 9.
Mzigo huo ulikuwa mzito sana kwa vijana wa Tanga kwani jitihada zao zote ziligota kwenye mikimbio 80 baada ya wote 10 kutolewa wakiwa wametumia mizunguko 20 kati ya 30 ya mchezo huo.
Kwa matokeo hayo, Vijana wa Azania wakatoka na ushindi mnono wa mikimbio 69.
Nyota wa mchezo alikuwa Arif Raja, ambaye peke yake alitengeneza mikimbio 62 kutokana na mipira 64.
Wengine waliochangia ushindi wa Azania ni Rehaan Atif ambaye alitengeneza mikimbio 33 kutokana na mipira 42 na Johnson David ambaye alipiga mikimbio 14 kutokana na mipira 21.
Mchezo mwingine wa Ligi ya TCA Inter-Academy ulishuhudiwa timu ya Dar Combine ikiwaadhibu Gairo Boys kwa ushindi mkubwa wa wiketi 8.
Vijana wa Gairo ndio walioanza kubeti, lakini walichoambulia ni mikimbio 54 tu baada ya wote kutolewa wakiwa wamemaliza mizunguko 13 kati ya 30 ya mchezo huo.
Ilikuwa kazi nyepesi sana kwa vijana wa Dar Combine, kwani iliwachukua mizunguko 9 tu kutengeneza mikimbio 55 na kushinda mechi wakiwa wamepoteza wiketi 2.
Ni matokeo hayo ndiyo yaliyowapa Dar Combine ushindi wa wiketi 8.
Sanay Jobanputra ndiye aliyewamaliza Gairo Boys baada ya kushinda kwa wiketi 5 huku akiwa pia ametengeneza mikimbio 9.
Kwa upande wa mikimbio, Dev Mandania ndiye alikuwa mbabe wa wote baada ya kutengeneza mikimbio 27 akifuatiwa na Prakash Chauhan aliyeiletea timu yake mikimbio 12 na pia kushinda wiketi 2.