Simba, Mtibwa goma lipo pale pale Manungu

HATIMAYE sintofahamu ya mchezo wa Mtibwa Sugar dhidi ya Simba kupigwa Uwanja wa Manungu imetatuliwa na watu wa usalama juu ya mtanange huo.
Ilielezwa kwamba jana Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliwatuma watu wa usalama kuangalia hali ya usalama kwenye uwanja huo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kesho Jumamosi baada ya ukarabati na timu hizo zikiwa zimecheza kwnye uwanjani hapo baada ya miaka 20 sasa.
Baada ya kuwepo kwa taarifa hizo, Mwanaspoti lilimtafuta Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya bodi hiyo, Karim Boimanda ambaye amesema, uwanja huo umezingatia taratibu na kila kitu kinachotakiwa na ndio maana wameruhusu mechi hiyo kuchezwa hapo huku na kwamba wameangalia mazingira ya uwanja na uuzaji tiketi ambavo vimekidhi vigezo vya kiusalama.
"Taarifa ni kwamba mazingira ya uwanja na uuzaji tiketi yanakidhi vigezo vya kiusalama. Zingatio ni kwamba idadi ya tiketi zitakazouzwa ni 2,500 tu na hakuna tiketi itauzwa kwa jukwaa la VIP, watu watakaoruhusiwa kufika eneo la uwanja ni wale tu wenye tiketi," amesema Boimanda.
Aidha Boimanda amesema, kutakuwa na vizuizi kwenye njia za kuelekea uwanjani hivyo usalama utakuwepo wa kutosha.
Mtibwa Sugar imekomalia mchezo huo kupigwa katika uwanja wao licha ya idadi kubwa ya mashabiki wa Simba lakini wao wamesema hawahitaji hata shabiki mmoja katika mchezo huo ilimradi uchezwe uwanjani hapo.