Dakika 45 za moto kwa Seleman Mwalimu

Muktasari:
- Mtanzania huyo aliyejiunga na Wydad Januari 2025, akitokea Singida Black Stars, aliingia kipindi cha pili kilipokuwa kinaanza akichukua nafasi ya Bart Meijers.
MSHAMBULIAJI wa Wydad Casablanca ya Morocco, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, amecheza mechi yake ya kwanza akiwa na timu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Juventus ya Italia, huku akikiri ni heshima kubwa kwake licha ya kupoteza.
Mtanzania huyo aliyejiunga na Wydad Januari 2025, akitokea Singida Black Stars, aliingia kipindi cha pili kilipokuwa kinaanza akichukua nafasi ya Bart Meijers.
Katika mechi hiyo ya kundi G, iliyopigwa Juni 22, 2025 kwenye Uwanja wa Lincoln Financial uliopo jiji la Philadelphia nchini Marekani, Wydad ilichapwa mabao 4-1, ikiwa ni kipigo cha pili mfululizo, baada ya awali kuchapwa 2-0 na Manchester City ya England.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gomez alisema kitendo cha kupata nafasi ya kucheza michuano hiyo mikubwa ni heshima kubwa kwake, kwani itabaki katika historia ya kumbukumbu nzuri za maisha aliyopitia.
“Imeniuma kwa sababu tumepoteza mechi mbili mfululizo ila sijaangalia sana hilo, isipokuwa nilichohitaji ni kupata fursa ya kucheza katika michuano hii mikubwa, kwangu imeniongezea morali ya kuamini kila kitu kinawezekana,” alisema Gomez.
Nyota huyo alisema michuano hiyo ina hadhi kubwa na hata wachezaji anaokutana nao pia wana uzoefu wa kutosha kutokana na timu wanazocheza, hivyo inamuongezea ile hali ya kujiamini na kuendelea kupambana zaidi kila anapopewa nafasi uwanjani.
Katika dakika hizo 45 alizocheza nyota huyo dhidi ya Juventus, kwa mujibu wa mtandao wa FotMob, aligusa mpira mara 15, akapiga pasi sita (6/6) ambazo zilifika zote kwa usahihi wa asilimia 100, alipiga shuti moja lililolenga lango la wapinzani (1/1) kwa usahihi wa asilimia 100 pia na kutengeneza nafasi ya hatari moja.
Takwimu za Gomez zinaonyesha amepata alama 6.8, akiwa mchezaji wa tatu wa Wydad aliyepewa alama nyingi katika mchezo huo baada ya mfungaji wa bao pekee Thembinkosi Lorch (7.7) na Nordin Amrabat (7.4) ambao walicheza kwa dakika zote 90.
Gomez wakati anajiunga na Wydad, alikuwa amefanya vizuri katika Ligi Kuu Bara alipokuwa akiitumikia Fountain Gate kwa mkopo akifunga mabao sita.
Wakati Gomez akifanya hivyo, Stephane Aziz KI ambaye alitua Wydad hivi karibuni akitokea Yanga, aliingia uwanjani katika dk87 kuchukua nafasi ya Fahd Moufi.
Kwa mujibu wa mtandao wa FotMob, Aziz KI katika dakika tatu alizocheza, alipiga shuti moja ambalo halikulenga lango na kutengeneza nafasi moja, huku akigusa mpira mara nane. Pia alipewa jukumu la kupiga kona akifanya hivyo mara mbili. Alipiga pasi sita (6/6) na zote zikafika kwa usahihi wa asilimia 100.
Wydad kwa sasa inashika nafasi ya tatu ikiwa haina pointi na tayari imeaga michuano hiyo, ikisubiri kucheza mechi ya kukamilisha ratiba ya kundi G dhidi ya Al Ain FC kutoka Falme za Kiarabu Juni 26 inayoburuza mkia.
Katika kundi hilo, tayari Juventus na Manchester City zimefuzu hatua ya 16 bora baada ya kukusanya pointi sita kila moja. Juventus inaongoza kundi kwa kufunga mabao tisa, Man City (manane).