Simba, Mashujaa gemu ya lawama

Muktasari:
- Kwa kiswahili cha kijiweni wanasema ni mechi ya lawama. Inahitaji akili nyingi kwa timu zote mbili, kwani wanatoka kwenye mapumziko wakiwa na usajili mpya. Vikosi vitakuwa ni vipya na ya ndani na nje ya Uwanja ni kubwa kusaka matokeo kwani hawako kwenye nafasi nzuri.
Achana kwanza na robo fainali za Afcon usiku. Jioni ya leo, Abdelhack Benchikha atakuwa na kibarua cha kwanza kwenye ligi nje ya Dar es Salaam tangu asaini Simba. Ataiongoza timu yake dhidi ya Mashujaa iliyosukwa upya ndani ya Lake Tanganyika, Kigoma.
Kwa kiswahili cha kijiweni wanasema ni mechi ya lawama. Inahitaji akili nyingi kwa timu zote mbili, kwani wanatoka kwenye mapumziko wakiwa na usajili mpya. Vikosi vitakuwa ni vipya na ya ndani na nje ya Uwanja ni kubwa kusaka matokeo kwani hawako kwenye nafasi nzuri.
Lolote linaweza kutokea ndani ya dakika 90. Lakini kwa aina ya wachezaji na uwanja wa mechi, makocha wataanza na vikosi vya kuondoa lawama. Watajilipua.
Simba ya Benchikha baada ya kucheza mechi mbili ndani ya jiji la Dar es Salaam kisha ikashinda mechi moja na kutoa sare moja, itakutana na wenyeji wao Mashujaa ambao inawajua fika ikizubaa kidogo tu wanajeshi hao wanatibua hesabu na kuibua lawama.

Rekodi zinakumbusha, timu hizi zimewahi kukutana mara mbili, ya kwanza ikiwa ni kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 64 iliyopigwa Desemba 26, 2018 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaa ambapo Simba ikachapika mabao 3-2 na kutupwa nje ya michuano. Lawama zikaanza. Lakini miezi michache baadae, Oktoba, 2019 zilikutana kwenye mechi ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika na Simba kuibuka na ushindi wa bao 1-0 la kiungo Msudan, Shiboub Sharraf Eldin. Mashujaa wakajilaumu, kwani walitaka kuendeleza ubabe kwa Simba.
Sasa leo zinakutana kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa Ligi Kuu. Huo ni mchezo wa 13 kwa Mashujaa. Imeshinda mechi mbili pekee tena zote za nyumbani itahitaji ushindi ili kuthibitisha usajili waliofanya hawakukosea. Vinginevyo, lawama zitaanza leo leo.
Mashujaa kwenye mechi hizo 12 zilizopita imepoteza saba na tatu ziliisha kwa sare na leo itahitaji ushindi ili kujiondoa nafasi ya pili kutoka mkiani mwa msimamo wa ligi, ili isirejee ilikotoka kwani mechi mbili zijazo na zenyewe zimekaa kilawama kweli kweli. Watazifuata Yanga na Dodoma ugenini.
Timu hiyo imefanya usajili mzito ikiingiza watu wapya 12 lakini mastaa ambao watabeba heshima ya timu hiyo ni sita, kiungo mshambuliaji, Abdulrahman Mussa, Reliants Lusajo, Balama Mapinduzi ambao wamewahi kuifunga Simba kwa nyakati tofauti na klabu zao za zamani huku kwenye ukuta ikiwaingiza wakali kama Ibrahim Ame ambaye ni beki wa zamani wa wekundu hao na Mpoki Mwakinyuke.
Ushindi wa mwisho wa Mashujaa ulikuwa Septemba 16, mwaka jana iliposhinda mabao 2-0 ikiwa Lake Tanganyika dhidi ya Ihefu. Baada ya hapo lawama zikaanza. Lakini walipoenda mapumziko wamesuka kikosi ambacho wanaamini sasa lawama basi.
Ukuta wa Mashujaa unavuja kabla ya ujio wa kina Ame na timu hiyo imeruhusu mabao 17 na huku safu yao ya ushambuliaji ikifunga mabao tisa tu, lakini kocha mkuu, Mohammed Baresi akizungumzia mchezo huo alisema kikosi chake kipo tayari kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni.
“Tumepata muda wa kutosha wa kujiandaa tunaamini sasa tupo tayari kuipigania timu kupata ushindi, tunafahamu ubora wa Simba tutacheza kwa tahadhari kubwa lakini tukiwa na hesabu za kutafuta mabao,” Baresi alisema.
Za ndaani kabisa ni Baresi kabla ya usajili wa dirisha dogo ilibaki kiduchu atimke kukimbia presha ya matokeo.
Simba imewaingiza washambuliaji wa kigeni Freddy Michael Kouablan, Pa Omar Jobe, wapo pia viungo washambuliaji wazawa watatu Edwin Balua, Ladack Chasambi na Saleh Karabaka huku pia yumo kiungo mkabaji Babacar Sarr.
Kwenye mechi tano zilizopita Simba bado haina mwendo mzuri sana, kwani imeshinda mbili, ikitoa sare mbili na kupoteza moja na sasa ikiendelea kujitafuta chini ya Benchikha.
Safu ya ushambuliaji ya Simba imefunga mabao 23 na kuamua kuanza mapya baada ya kumtema aliyekuwa mshambuliaji kinara wa mabao, Jean Baleke aliyefunga manane kati ya hayo 23. Ukuta wao pia haujatulia ukiwa umeruhusu mabao 13 na leo itamkosa beki wake wa kazi Henock Inonga ambaye jana alikuwa uwanjani Ivory Coast ilipokuwa inapambana dhidi ya Guinea hatua ya robo fainali ya Afcon.
Simba inahitaji ushindi wa nane msimu huu ambao hata ikiupata utaifanya kuongeza alama tatu na kufikisha 26 lakini itabaki hapo hapo nafasi ya tatu ikiendelea kuifukuza Yanga yenye pointi 31 nafasi ya pili.
Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola alisema, “Tunafahamu Mashujaa naweza kuwa na kikosi tofauti na kile ambacho kilikuwa kinacheza kabla ya kusimama kwa ligi, mchezo utakuwa mgumu kwa timu zote lakini tunazihitaji alama tatu ambazo zitatuongezea kitu kwenye malengo yetu kabla ya kwenda kucheza mechi nyingine ngumu ugenini,” alisema Matola ambaye ni kiungo na nahodha wa zamani wa wekundu hao.