Simba kuzoa fedha za Caf
Muktasari:
Simba itacheza Jumatano na wageni wao, FC Platnum.
Dar es Salaam. Siku tatu zimebaki kabla ya Simba kufahamu hatma yake katika Ligi ya mabingwa Afrika kama watasonga katika hatua ya makundi au wataishia hapo, kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya FC Platinum kutokea Zimbabwe ambao mechi ya kwanza walishinda bao 1-0, wakiwa nyumbani kwao.
Shirikisho la soka Afrika (CAF), ambalo linaandaa mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu linaonyesha kuwa timu 16, ambazo zitatinga hatua ya makundi wanajihakikishia kuchukua Dola za kimarekani 550,000, sawa na Sh1.2 bilioni bila kujali kama watafuzu robo fainali.
Simba kama watafanikiwa kutinga hatua ya makundi na wakafanya vizuri na kufika robo fainali kama ilivyokuwa mwaka juzi CAF, watawaongezea fedha hizo na kufika, Dola 600,000 (Sh1.3 bilioni).
Fedha hizo zote ambazo CAF, wanazitoa ni kwa ajili ya maandalizi ya kila timu katika mahitaji yake ya msingi kama nauli ya kutoka eneo moja kwenda lingine, posho kwa wachezaji na benchi la ufundi, kuweka kambi mahala ambapo wanahitaji pamoja na mambo mengine yote ya msingi.
Kama Simba watatinga katika hatua hiyo ya makundi au kusonga mbele itakuwa faida na heshima kwa timu, mchezaji mmoja mmoja na kuweka rekodi nyingine kwa kizazi cha sasa kufika hatua ya makundi kwenye mashindano hayo katika miaka ya karibuni.
Mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere alisema pesa hiyo ambayo inatolewa na CAF, inaongeza maroli ya kila timu kushindana kadri ambavyo wanaweza katika mashindano hayo ili kufika mbali ndio maana kuna baadhi ya timu malengo yao ya kwanza ni Ligi ya Mabingwa.
“Mashindano haya ni makubwa kwanza kufika katika hatua ya makundi itakuwa heshima kubwa kwetu na ambavyo kikosi chetu kilicho jambo hilo linawezekana, kuhusu bonasi inasaidia kwetu kwani inafanya morali kuwa juu na hilo viongozi wetu wamekuwa wanalifanyia kazi vizuri,” alisema Kagere.
Kiungo wa Simba, Mzambia Larry Bwalya alisema pesa hiyo ambayo inatolewa kimsingi lazima kuna ahadi itakuwa inakwenda kwa wachezaji na kwa hali ya kawaida lazima kuna morali ambayo itakuwa inaongezeka kwao.
Ushindi ndiyo kitu cha msingi zaidi bila kuangalia nini tutakipata kutokana na kutinga hatua ya makundi,” alisema Bwalya.
Beki wa kati wa Simba, Ibrahim Ame alisema motisha ya pesa kama bonansi ambayo wanaipata mara baada ya kushinda michezo ya ligi ni nyingi na inawasaidia katika mambo ya ya kimaisha itakuaje hiyo nyingi zaidi ambayo inaelezwa na CAF, maana yake wanatakiwa kupambana kuliko kawaida.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema kuwa timu yake imejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo.