Kagere: Kwa Simba hii mbona yeyote anakutungua
JUZI katika mechi ya Ligi Kuu Bara, Simba tuliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Ihefu SC, huku nikifanikiwa kufunga mabao mawili, na kukosa nafasi nyingine kadhaa ambazo zingetunisha akaunti yangu ya mabao.
Mabao hayo mawili niliyofunga kwenye mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, yamenifanya nifikishe jumla ya mabao saba, nikilingana na Adam Adam wa JKT Tanzania, tukiwa nyuma ya kinara wa mabao na nahodha John Bocco, aliye majeruhi kwa sasa kikosini.
Katika kolamu yangu wiki hii ningependa kuzungumzia jambo hilo la kufikisha idadi ya mabao saba huku nikiwa nyuma ya bao moja ni nahodha wangu Bocco ambaye ndio anaongoza msimamo wa wafungaji.
Kwanza ni jambo la faraja mno kuona nahodha wangu ndio kinara wa ufungaji katika ligi na hii inaonesha mbali ya kuwa kama kiongozi ndani ya timu anatimiza majukumu yake kwa vitendo kwa maana ya kwenda kufanya yale ambayo ambayo anaagizwa na benchi la ufundi uwanjani.
Jambo lingine inaonesha kiasi gani safu yetu ya ushambuliaji inawachezaji ambao wanatimiza majukumu yao ipasavyo kwani si mimi niliyefunga mabao saba au Bocco mwenye nane kwani kuna wengine kama Chriss Mugalu, Clatous Chama, Luis Jose Miquissone nayo mabao mengi.
Tofauti na hilo kunakuwepo na hamu ya kucheza kwa kila mmoja anayepata nafasi ya kutumika katika mechi husika ana kuwa na kiu ya kufanya vizuri kwa kutimiza majukumu yake ndio maana kila unapotuona tukicheza kwa pamoja au wawili na hata mmoja tunafunga kila mara.
Binafsi kwetu hakuna ushindani bali tumekuwa tukipeana nguvu na kuelekezana kwa yule ambaye anapewa nafasi ya kucheza ili kwenda kurahisisha ushindi wa timu kwa maana ya kufunga mabao kila ambavyo atakuwa anapata nafasi ya kucheza.
Binafsi kwa upande wangu mabao mawili ambayo nimefunga katika mchezo uliopita dhidi ya Ihefu umeongeza morali ya kutamani kufunga zaidi kila ambapo nitapata nafasi ya kufanya hivyo ili kuishi katika ndoto yangu ambayo nimekuwa nikiitamani na kuieleza wakati wote.
Ndoto yangu kubwa ambayo nimekuwa nikieleza msimu huu natamani kwanza kumaliza nikiwa na idadi ya mabao 22, ambayo niliyafikia msimu uliopita bila ya kujali kama nitaweza kuwa mfungaji bora au sitakuwa.
Baada ya kufikia idadi ya mabao hayo ndio nitakuwa na malengo mengine ya kuongeza mabao ikiwemo kufikia idadi ya mabao 23, niliyofunga msimu wangu wa kwanza kucheza katika ligi ya Tanzania na jambo hilo linawezekana kutokana na timu yetu ilivyo.
Ambacho ninachoamini kama Kagere nikiweza kutimiza majukumu yangu ya kufunga kama ambavyo wanafanya wachezaji wengine katika kikosi hiki kutakuwa na faida nyingi ikiwemo kurahisisha safari yetu ya ubingwa ambayo ndio malengo makuu katika kwetu.
Lakini ambalo natamani kulifanya na naliona mbele yangu kwanza Simba tunatakiwa kuipigania wachezaji wote ili kufikia malengo kama kuchukua ubingwa wa ligi, kufika mbali katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuchukua mataji mengine mbalimbali ambayo tutakuwa tunashiriki.
Kimsingi Simba tumebakiwa na mechi 19, kabla ya kumaliza msimu na kama nitakuwa naendelea kupata nafasi ya kucheza na kutumika idadi ya mabao ambayo nataka kufunga si kubwa naamini nia ninayo na uwezo wa kufikia hayo upo.
Ushirikiano ambao naupata kutoka kwa wachezaji wengi kwa kila mmoja kutimiza majukumu yake unaongeza morali na hali ya kujimini kama naweza kufikia malengo yangu na yale ambayo tunahitaji kiujumla kama timu.
Ujua kila mchezaji anaweza kukutana na wakati mgumu katika kipindi chake cha kucheza soka kuna wakati anakuwa bora lakini muda mwingine anakutana na changamoto za kushindwa kufanya vizuri hilo nalo linawakumba kwa upande wao lakini wamejipanga kulipatia majibu.
Ukiachana na hilo katika Ligi ya Mabingwa msimu wangu wa kwanza kuitumikia Simba nilifunga mabao sita mawili moja nyuma ya aliyekuwa mfungaji bora ni miongoni mwa rekodi ambayo nimekuwa nikiitamani kuifikia muda wote.
Bado Simba tupo katika mashindano haya ya kimataifa si kazi rahisi, lakini naamini kwa ubora wa kikosi chetu kilivyo na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja malengo kwanza ni kufika mbali na hayo mengine yatafuata kama ilivyokuwa katiki nafikisha idadi hiyo.
Kwa maana hiyo nawaomba kwanza mashabiki na wepenzi wetu kuendelea kutupa nguvu kila tunapocheza kama katika mechi na FC Platinum ambayo inafuata ili kupata aina ya matokeo ambayo yatatuvusha katika hatua inayofuata na ndani yake ndio tutapata nafasi ya kufunga.
Unajua katika mechi hiyo ili tushinde lazima tufunge mabao na hilo linawezekana haswa tukiwa tunapata nguvu ya kuhamasishwa na mashabiki wetu watakaokuwa wamejitokeza kwa wingi uwanjani kwani kucheza huku unapata nguvu ya kushangiliwa inaongeza hali ya kushindana.
Imeandikwa na Meddie Kagere, Simba