Simba kutozwa faini kukacha kikao

Muktasari:
- Mapema leo asubuhi Simba imeshindwa kutokea kwenye mkutano wa makocha na wanahabari uliofanyika makao makuu mdhamini wa ligi hiyo huku Yanga ikitokea.
KUELEKEA mchezo wa Dabi ya Kariakoo, Simba imeshindwa kutokea katika mkutano wa pili wa maandalizi ya mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa kesho kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam hivyo itapigwa faini ya Sh500,000.
Mapema leo asubuhi Simba imeshindwa kutokea kwenye mkutano wa makocha na wanahabari uliofanyika makao makuu mdhamini wa ligi hiyo huku Yanga ikitokea.
Mkutano huo wa kikanuni uliwataka makocha na manahodha wa timu hizo kuzungumza na wanahabari kuelekea mchezo huo ambao utapigwa kesho.
Timu hiyo imeshindwa kutokea kwenye mkutano wa maandalizi ya mchezo kati ya maofisa wanaosimamia mchezo huo uliofanyika Hoteli ya Tiffany jijni Dar es Salaam.
Yanga imefika kwenye hoteli hiyo, kisha kukutana na mtathmini wa waamuzi kutoka Somalia, Alli Mohamed na kamishna wa mchezo huo, Salim Singano.
Hata hivyo, waamuzi wa mchezo huo, Amin Omar ambaye ni mwamuzi wa kati na wasaidizi wake, Mahmoud El Regal na Samir Mohamed wote kutoka Misri hawakuwa sehemu ya mkutano huo.
Simba itakumbana na adhabu nyingine ya faini sambamba na kushindwa kupewa nafasi ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mchezo kwa kushindwa kuwasilisha ratiba kwenye kikao hicho.