Simba kutesti na Mazembe Dar

MABOSI wa Simba jana wamemshusha kocha wa makipa, huku wakimsainisha kiungo fundi kutoka DR Congo, Doxa Gikanji, wakati wakimsubiri kocha mkuu mpya kutua nchini kuanzia leo ili kuwahi kuliamsha dude katika michuano maalumu itakayoanza Jumanne.
Katika michuano hiyo, Mwanaspoti limepenyezewa kuwa Simba imezialika timu za TP Mazembe ya DR Congo, Al Hilal ya Sudan na Azam iliyokuwa kambini visiwani Zanzibar ikicheza mechi za kirafiki tangu ilipotolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021.
Chanzo makini kutoka ndani ya Simba kinasema kuwa, michuano hiyo itatumika kama nafasi ya Kocha Mkuu atakayechukua nafasi ya Sven Vandenbroeck aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco ambaye anatarajiwa kushuka nchini kuanzia leo ili kuungana na wachezaji kambini Jumatatu.
“Kila kitu kuhusu makocha kimekamilika, anaweza kutoka Afrika Kusini ama Misri, kwani ndio majina ya mwisho yaliyokuwa yakijadiliwa, ila kocha wa makipa ameshatua na jana alikuwa akimalizana na mabosi ili kuanza kazi sambamba na kocha mkuu Jumatatu kambi itakapoanza.”
Chanzo hicho kiliongeza kuwa, michuano hiyo maalumu ya Simba ni kama ile iliyokuwa ikifanywa na klabu ya Arsenal iliyofahamika kama Emirates Cup na lengo ni kuziweka tayari timu shiriki kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu za ndani.
Mazembe, Al Hilal kama Simba, zote zimetinga hatua ya makundi, wakati Azam inajiandaa na Ligi Kuu, japo Ofisa Habari wake, Thabit Zakaria alipoulizwa jana juu ya michuano hiyo maalum ya Simba alisema hana taarifa nayo.
“Sina taarifa zozote za michuano hiyo, kwani tupo Zanzibar na kambi tumevunja leo, wachezaji wa Bara na baadhi ya viongozi tunarejea kesho, kwani 2wachezaji wamepewa mapumziko mafupi hadi Jumatatu kambi itakapoanza upya,” alisema Zakaria maarufu kama Zaka Zakazi.
Hakuna kiongozi wa Simba aliyepatikana kuthibitisha taarifa za michuano hiyo, kwani simu zao zilikuwa zikiita bila kupokelewa, ikielezwa walikuwa wakimalizana na kocha wa makipa aliyetua jana na kwenda kuonana na mabosi hao akiwamo Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, pia kupambana ili kocha mkuu mpya awahi kabla ya Jumapili.
YANASA KIUNGO
Katika hatua nyingine Simba imezidi kuimarisha kikosi kwa kumnasa kiungo mkabaji kutoka DC Motema Pembe ya DR Congo, Doxa Gikanji mwenye umri wa miaka 30, huku jina la Taddeo Lwanga likikosekana kwenye orodha ya wachezaji wa Simba waliosajiliwa dirisha dogo kwa wachezaji wa Ligi Kuu Bara.
Lwanga alipoulizwa juu ya kukosekana kwa jina lake, alionekana kushangaa akidai yupo njiani kwani alisajiliwa kama mchezaji huru kwa michuano yote ya ndani na ya kimataifa na alishapewa tiketi ya kwenda kwao Uganda na kurudi, akitarajiwa kuingia nchini Jumapili kuwani kambi.
“Ndio kwanza nasikia kwako kwamba jina langu halipo, wakati nilisajiliwa mapema na kuanza kuichezea, ila natarajia kurejea nchini Jumapili,” alisema Lwanga kwa kifupi, Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura alipoulizwa juu ya kutoonekana kwa jina la Lwanga na kuonekana la Gikanji alisema; “Hii ndio orodha ya waliosajiliwa dirisha dogo na tumetoa kwa ajili ya mapingamizi, kama jina la mchezaji halionekani, ujue hajasajiliwa na timu husika kwa ligi ya ndani,” alisema.
Hata hivyo, Simba imefanya usajili wake kwa minajili ya wachezaji wa kuichezea Ligi ya Mabingwa Afrika akiwamo Junior Lokosa, huku wengine wakisajiliwa kwa ligi ya ndani na hii ni baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuongeza idadi ya nyota kutokana na janga la corona. Usajili wa CAF kwa sasa unaendelea mpaka mwishoni mwa mwezi huo.
Kiungo mpya aliyenaswa na Simba aliyezaliwa Agosti 21, 1990 anasifika kwa kukaba na kutoa pasi mbali na kupiga mashuti makali na kufunga na amewahi kukipiga timu za TP Mazembe na DC Virunga na pia kuichezea timu ya taifa ya DR Congo tangu mwaka 2015.
Mbali na kumudu kiungo cha kukaba, Gikanji anaweza pia kucheza kama kiungo mshambuliaji na hivi karibuni aliongezwa kwenye orodha ya wachezaji wa timu ya DR Congo iliyopo Cameroon inaposhiriki Fainali za CHAN 2021.