Simba kushusha mziki mnene kesho

Kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema kesho Jumamosi huenda nyota wake kibao wakaonekana kwenye mechi yao ya pili watakapoivaa Mtibwa Sugar.
Mechi hiyo ni ya pili kwa timu hizo katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoendelea kisiwani hapa ambapo Mtibwa Ilishindwa mechi ya kwanza dhidi ya Chipukizi bao 1-0 huku Simba nayo ikiifunga Chipukizi bao 3-1.

Katika mchezo huo, Chipukizi ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 35 lililifungwa na Faki Sharif baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Simba huku kipa wao Beno Kakolanya akishindwa la kufanya.
Meddie Kagere aliisawazishia Simba dakika ya 44 akipokea krosi iliyopigwa na David Kameta 'Duchu' ambaye alikosa pia dakika ya 45 baada ya kupiga shuti lililotoka nje kidogo ya goli.
Matokeo hayo yalizifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1 lakini baada ya mapumziko Simba walirudi na kasi ambapo dakika ya 52, Miraji Athuman aliifungia bao la pili timu yake akipokea krosi ya Kagere na kuongeza bao la tatu dakika ya 82 akipokea pasi ya Duchu.
Hata hivyo Simba ilikosa bao kipindi cha kwanza kabisa dakika ya sita baada ya Hassan Dilunga kupiga mpira huko pasi ikiwa ni ya Gadiel Michael huku wapinzaji wao nao wakijaribu kufanya shambulizi langoni mwa Simba dakika ya 25.
Dakika ya 56, Chipukizi chupuchupu wajifunge kutokana na kutaka kuokoa shambulizi langoni mwao lakini baadaye mpira uliokolewa kwa kuupiga nje ya goli.
Matola alifanya mabadiliko ya wachezaji wake ambapo aliingia Francis Kahata akitoka Nyoni huku Lwanga naye akipumzishwa nafasi yake ilichukuliwa na Mzamiru Yassin, alitoka Ibrahim Ajibu nafasi yake ilichukuliwa na Cyplian Kipenye, mabadiliko hayo yalifanyika kipindi cha pili.
Naye kocha wa Chipukizi, Mzee Ali Abdallah akimtoa Khamis Mohamed Hassan nafasi yake ilichukuliwa na Kassim Salim.
Miraji mchezaji bora
Jopo la kamati ya mashindano ilimchagua Miraji kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, ambapo kila mechi kwenye mashindano hayo huchaguliwa mchezaji bora.

Akizungumza mara baada ya mechi hiyo, Matola amesema kuwa; "Nimebadilisha kikosi kwasababu wengine walichoka kutokana na majukumu tuliyokuwa nayo, hivyo wasishangae kesho wakacheza maana mechi ya kesho ina ushindani mkubwa.
"Ni mechi ngumu na ikumbukwe ndiyo waliotutoa mwaka jana, hivyo lazima kujiandaa kupambana na kushinda ili kusonga mbele, mechi ya leo (Ijumaa) wamecheza vizuri na wamepata kile tulichokikusudia," amesema Matola