Simba kuitibulia tena Al Ahly

Sunday February 28 2021
simba pic ahly
By Khatimu Naheka

SIMBA inaendelea kutamba mitaani kutokana na matokeo ya kuipiga Al Ahly yenye rekodi ya mataji mengi duniani lakini kipigo hicho cha pili kwa Waarabu hao ndani ya msimu huu kinaweza kuwatibulia tena kutetea ubingwa wao wa Afrika.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Al Ahly imekuja nchini mara tatu na kupoteza, wakianza mwaka 2014 wakapoteza mbele ya Yanga kwa bao 1-0 likifungwa kwa kichwa na aliyekuwa beki na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyemaliza kona ya Simon Msuva.

Hata hivyo, Yanga ilipoenda ugenini ilifungwa pia bao 1-0 na kutolewa kwa penalti 4-3, lakini ni licha ya Al Ahly kuing’oa Yanga haikufika fainali ya Afrika kwani ilitolewa na Al-Ahly Benghazi kwa jumla ya mabao 4-2 katika hatua ya pili na ES Setif ya Algeria ikabeba taji.

Mwaka 2019 Ahly walitua tena nchini safari hii wakikutana na Simba katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo baada ya kuifunga Simba mabao 5-0 wakajikuta wakipogea kipigo cha kushtua cha bao 1-0, lililowekwa kimiani na straika Meddie Kagere.

Hata hivyo, Ahly iliongoza Kundi D akivuna pointi 10 ikifuatiwa Simba iliyokuwa na alama tisa, lakini waarabu hao tena hawakufika fainali kwani walipoteza kwenye robo fainali kwa kutolewa na Mamelodi Sundowns iliyokuwa chini ya kocha wao wa sasa, Pitso Mosimane.

Msimu huo mabingwa walikuwa ni Wydad Casablanca iliyowazidi ujanja Esperance ya Tunisia.

Advertisement

Hivyo kwa msimu huu baada ya kufumuliwa na Simba, Al Ahly kama wasipokaza wanaweza kukutana na gundu la miaka yote wanapokuja nchini na kufungwa, kisha kushindwa kubeba ubingwa wa Afrika.

Hata hivyo, ni kwenye Ligi ya Mabingwa tu, Waarabu hao walipofungwa na timu ya Tanzania walikwama njiani, lakini rekodi zinaonyesha mwaka 1985 katika Kombe la Washindi walifungwa na Simba 2-1 jijini Mwanza kwa mabao ya Zamaoyoni Mogella na Mtemi Ramadhani, lakini wababe hao walienda kubeba ubingwa kwa kuinyoa Leventis United ya Nigeria katika mechi za fainali.

Advertisement