Bao la Miquissone laisafishia Simba

Dar es Salaam. Simba inahitaji pointi nne kujihakikishia kutinga katika hatua ya robo fainali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Baada ya kuibuka na ushindi wa ugenini wa bao 1-0 dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo, miamba hiyo ya soka nchini iliibuka pia na ushindi kama huo dhidi ya vigogo wa Afrika, Al Ahly.

Bao la mshambuliaji wa kimataifa wa Msumbuji, Luis Miquissone lilitosha kuipa Simba ushindi dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Mkapa, na kujiimarisha kileleni mwa Kundi A.

Simba inaweza kujihakikishia nafasi nzuri kabla ya mechi mbili za mwisho itakapoifuta El Merreikh ya Sudan katika mchezo ujao wa Kundi A, ambao utawasogeza mabingwa hao karibu na robo fainali.

Pointi 10 kutoka katika kundi lao linaweza kuipa Simba nafasi kutokana na Al Ahly na AS Vita kushika nafasi ya pili na tatu kwa kuwa na pointi tatu.

Simba yenye pointi sita inapewa nafasi ya kusonga mbele mapema zaidi kama itafanikiwa kuifunga El Merreih mwezi ujao, ambao wanaburuza mkia kwa kufungwa mechi zote mbili za kwanza.

Lakini gumzo zaidi lilikuwa bao la kuifundi la Miquissone, ambalo aliifunga Al Ahl;y kwenye Uwanja wa Mkapa, juzi, baada ya kugeuka na kupiga shuti la mguu wa kulia lililotinga katika kona ya mbali ya lango.

Kipa wa zamani wa Simba, Mohammed Mwameja alisema hakuna kipa wa mpira wa miguu ambaye angeweza kuufuata mpira ule kutokana na kasi na umbali wa aliposimama kipa wa Al Ahly, El Shenawy.

“Hakuna kipa mwenye uwezo wa kudaka mipira ya aina hiyo, labda apangue tena napo inategemea,” alisema Mohammed Mwameja kipa wa zamani wa Simba wakati akilichambua bao hilo.

Mwameja alisema magoli ya aina hiyo yanafungwa na wachezaji wenye vipaji na mara nyingi makipa wanashtukizwa.

“Bao kama alilofunga Miquissone huwa ni mabao ya ubunifu sana, ndiyo mabao ambayo kina Lionel Mesi wanafunga, kipa mara nyingi anafungwa kwa kustukizwa na ndivyo ilikuwa hata kwa kipa wa ya Al Ahly, hakutarajia Miquissone angepiga shuti lile,” alisema Mwameja.

Nyota wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema bao lile ni uwezo binafsi wa mchezaji, Miquissone amelitengeneza mwenyewe bao lile na kufunga tena katika mazingira ambayo hata kipa wa timu pinzani hakutarajia.

“Miquissone aligeuka na ku ‘kevu’ upande mwingine na kupiga shuti, tukio ambalo kipa wa Al Ahly hakulitarajia na alistukizwa, magoli kama yale mara nyingi yanafungwa na wachezaji wabunifu,” alisema Mayay.

Mchambuzi wa soka, Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’ alisema bao hilo linaonyesha kiwango cha uelewa wa mpira kwa mchezaji.

“Kabla ya kufunga aliusoma kwanza ukuta wa mabeki wa Al Ahly wenye wachezaji wenye miili mikubwa, akili na utulivu wa mpira. Kwa namna walivyogongeana na Chama, kasha akageuka ghafla kipa hakutarajia kwamba atapata ujasiri wa kupiga kutoka pale.

“Kule kugeuka kumeonyesha ubunifu, ni wachezaji wachache wanafanya hivyo,” alisema.

Akizungumzia kiwango cha wachezaji wa Simba katika mechi hiyo, Kashasha alisema timu ilicheza vizuri huku Mwameja akiipongeza beki yote ya Simba kwa kufanya kazi yao ipasavyo.

Kipa mwingine wa zamani wa timu hiyo, Moses Mkandawile alisema katika mechi ya jana amebaini kuna tofauti ya aina ya uchezaji kwenye kikosi cha Gomes.