Simba, JKT Tanzania ni vita vya heshima

Muktasari:

Ushindi kwa Simba utakuwa faida zaidi kwao katika upunguza pengo la pointi walilonalo dhidi ya Yanga inayoongoza kwenye msimamo wa ligi.

Dar es Salaam. Kikosi cha Simba kinashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kucheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania.

Simba katika mchezo huu wanahitaji huku wakicheza kwa tahadhari kwa timu hizi mbili zina historia ya kusumbuana katika michezo yao.

Msimu uliopita, katika mchezo uliofanyika Agosti 29, JKT Tanzania wakiwa wenyeji walifungwa na Simba mabao 3-1 na katika mchezo wa marudiano uliochezwa Februari 7, Simba wakiwa wenyeji walifungwa 1-0.

Katika msimu huu, Simba iliichapa JKT Tanzania wakiwa nyumbani kwa mabao 4-0 mchezo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Oktoba 4.

Kocha wa Simba, Didier Gomes alisema katika msimu huu kila mechi kwao ni fainali kwani wanahitaji makombe yote.

“Kila mchezo ambao upo mbele yetu ni fainali, mechi zote tunazipa uzito iwe Ligi Kuu, Kombe la FA au Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Gomes.

Kwa upande wake, Kocha wa JKT Tanzania, Abdallah Mohamed ‘Bares’ alisema anatambua ugumu wa mchezo huo kulingana na kiwango cha wapinzani wao.

“Najua nakwenda kukutana na timu ngumu na wana washambuliaji wazuri, lakini nimeshawapa mbinu wachezaji wangu jinis ya kukabiliana nao.

“Najua Simba wanahitaji matokeo na sisi tunahitaji matokeo, tumemaliza mazoezi ya mwisho (jana asubuhi), kilichobaki ni wachezaji kufanya nilichowaelekeza,” alisema Bares.

Simba wanahitaji ushindi katika mchezo huo ili kupunguza pengo la pointi walilonalo na Yanga, ambao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 49 kwenye mechi 21, Simbani ya pili kwa pointi 42 katika mechi 18.

Simba inatarajia kuondoka nchini Jumanne kwenda Sudan kuivaa Al Mereikh kwenye mchezo wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika.