Simba ipo hatarini kama hawa

Muktasari:

  • Hatari inayoikabili ni kutokuwepo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikiwa itaendelea kupata matokeo  inayoyapata.

Mambo yanaonekana kuwa magumu kwa Simba. Msimamo wa Ligi Kuu Bara unaonyesha ipo nafasi ya tatu kwa pointi 46 ilizokusanya katika mechi 20.

Hatari inayoikabili ni kutokuwepo katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikiwa itaendelea kupata matokeo  inayoyapata.

Ili kufuzu michuano hiyo Simba itatakiwa kumaliza nafasi mbili za juu ambazo kwa sasa zinashikiliwa na Yanga na Azam yenye pointi 50 ilizokusanya katika mechi 22, hivyo tofauti  na Simba ni pointi nne, lakini wana lambalamba wamecheza mechi mbili zaidi.

Jambo gumu zaidi kwa Simba ni kwamba mechi mbili zinazofuatia itakutana na ugumu zaidi kwao ikianzia kwa Yanga, kisha Azam ambazo zimeonyesha kiwango bora kuzidi wao katika michezo mitano ya mwisho.

Simba haina matokeo mazuri kwa siku za hivi karibuni kwani haijapata ushindi wowote katika mechi nne zilizopita za michuano yote wakati Azam imeshinda mechi nne kati ya tano za mwisho.

Kutokana na pengo la alama kati yao na wapinzani wao wa jadi Yanga, Simba inataka kujihakikishia kumaliza nafasi mbili za juu mbali ya yote kwa kupambana na Azam ili kufuzu Ligi ya Mabingwa, lakini inaonekana kuwa ngumu kutokana na fomu na mechi zinazofuata kwa wababe hao wa Msimbazi.

Lakini sio Simba tu ambayo ipo katika hatari ya kutoonekana katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, katika zile timu zilizofuzu hatua ya makundi msimu huu, kwani vigogo wa Morocco, Wydad Casablanca wameshaaga kabisa.

Hadi sasa utofauti wa alama kati yao na Raja Casablanca inayoshika nafasi ya pili ni 20, Wydad inashika nafasi ya tano na zimebaki mechi tano kabla ya msimu kumalizika, hivyo hata ikishinda mechi zote itafikisha pointi 52 ambazo hazitaifikia Raja yenye pointi 57.

Etoile du Sahel ya Tunisia ambayo msimu huu imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, msimu ujao ipo katika hatari ya kutoshiriki.

Hadi sasa katika Ligi Kuu Tunisia ambayo ipo hatua ya pili inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi nne.

Ili kufuzu itatakiwa kumaliza katika nafasi mbili za juu ambapo hadi sasa utofauti wa pointi kati yao na US Monastir inayoshika nafasi hiyo ni pointi moja.

Ligi ya Tunisia mfumo wake unaanzia katika msimu wa kawaida na baada ya hapo timu sita za juu zinacheza ligi yao kumtafuta bingwa na timu zitakazofuzu michuano ya kimatafa na zile nane za mwisho zinacheza ligi kwa ajili ya kutafuta mbili zitakazoshuka daraja.

Etoile imewahi kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika 2017.

Medeama pia hali ni tete kwani hadi sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Ghana ikiwa na pointi 39, tofauti yake na Nations inayoshika nafasi ya pili ni pointi tano.

Medeama iliyomaliza nafasi ya mwisho katika hatua ya makundi itakuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha inarudi tena katika michuano hiyo mwakani, kwani imekuwa na panda shuka nyingi na mechi tano za mwisho za ligi hiyo imeshinda mbili, ikafungwa tatu na kutoka sare moja.