Kipa Kagera Sugar akiri walichemsha mapema

Muktasari:
- Kagera Sugar imeshuka daraja kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda Ligi Kuu miaka 21 iliyopita.
KIPA wa Kagera Sugar, Ramadhan Chalamanda amesema kushuka daraja kwa timu hiyo ni sawa na kifo kwa mwanadamu, lakini si kiwango kidogo kwa wachezaji, huku akifichua kushindwa kujipanga mapema na kuzinduka mwishoni ndiko kulikowagharimu.
Kagera Sugar imeshuka daraja kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda Ligi Kuu miaka 21 iliyopita.
Pamoja na kushuka daraja, bado ina mechi mbili za kuhitimisha msimu dhidi ya Namungo na Simba, zote ikicheza ugenini.
Chalamanda aliyeitumikia timu hiyo tangu 2017-2018 akitokea Madini ya Arusha, amekuwa na uhakika wa namba kikosini.
Akizungumza na Mwanaspoti, Chalamanda alisema matokeo waliyopata yamewashtua na kwamba wanaona sawa na kifo kwa mwanadamu kumtokea yeyote wakati unapofika.
Alisema licha ya kushuka daraja, lakini si kwamba hawakuwa na kiwango bora akieleza kuwa kwa sasa wanasubiri kumaliza mechi zilizobaki na kujipanga upya na msimu ujao kuona wataibukia wapi.
“Ni maumivu makali kushusha timu, tulipambana kwa uwezo wetu lakini ilipangwa iwe hivyo, hatuna namna, tunasbiri kumaliza mechi zilizobaki kisha kujipanga upya na msimu ujao,” alisema kipa huyo na kuongeza.
“Binafsi mkataba unaisha mwisho wa msimu huu, nitakapopata nafasi naweza kucheza kwani sichagui timu ya kufanya nayo kazi, uwezo na uzoefu ninao na popote naamini nitafanya vizuri.”