Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba ilikata roho kistaarabu, kukabaki Kiyangayanga

Wachezaji wa Simba na Yanga wakipeana mikono kabla ya kuanza kwa mechi yao iliyochezeka juzi katika Uwanja wa Taifa.

Muktasari:

Amefedheheka na kile alichokuwa anakitazama. Sura yake ilikuwa imevimba. Yanga walikuwa wanaongoza mabao 2-0.

DAKIKA ya 85, kamera za Azam TV zilimvuta kwa karibu Crescentius Magori, mmoja kati ya marafiki wa Simba. Alikuwa amekasirika.

Amefedheheka na kile alichokuwa anakitazama. Sura yake ilikuwa imevimba. Yanga walikuwa wanaongoza mabao 2-0.

Kando yake alikuwepo Geofrey Nyange Kaburu aliyekuwa ameshika tama, mikono juu ya kichwa. Shabiki mwingine wa Simba, Salim Abdaallah ‘Try again’ alikuwa amenyanyuka akiondoka huku vigogo wachache wakimshauri abaki kwa kuamini kuwa kwa dakika chache zilizobaki maajabu yangeweza kutokea.

Hakukuwa na maajabu. Hata mwamuzi Israel Nkongo ambaye alichezesha pambano hilo kwa dakika 100 alijua kwamba kusingekuwa na maajabu mengine zaidi. Simba alikuwa amelala kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu wa kuinyanyasa Yanga miaka ya karibuni.

Mechi ilianza na ilichezwa kwa staili ile ile ya miaka ya karibuni ambayo tumeizoea. Yanga walikuwa wanatetemeka kama kawaida yao.

Ndani ya dakika tatu tu, Kevin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ walikuwa wamegongana hewani bila ya sababu. Ally Mustapha ‘Barthez’ alisingizia kuumia na Haji Mwinyi alikuwa akibutua.

Kabla ya mechi, Simba walikuwa wanaamini kuwa wataifunga Yanga. Hata mashabiki wa Yanga hawakuwa na uhakika na timu yao. Huwa wana uhakika na timu yao pindi inapocheza na JKT Ruvu, Coastal, Azam, Mbeya City na wengineo. Lakini wanapocheza na Simba huwa wanamwagiwa maji.

Ni tatizo la kisaikolojia. Kadri mechi ilivyokuwa inakwenda ilionekana wazi kwamba historia ilikuwa inaelekea kujirudia. Zaidi inajulikana kuwa Yanga wanapenda kucheza pembeni, Simba wanajaza viungo wengi kati.

Kabla ya mechi ya juzi, Simba walikuwa wamempania kiungo wa Yanga, Thabani Kamukoso ambaye ameanza kung’ara. Ilikuwa ni akili rahisi tu kwamba Yanga ukiwajazia viungo wengi wanachanganyikiwa. Ndiyo maana Simba ilianza na Said Ndemla, Justice Majabvi, Mwinyi kazimoto na Awadhi Juma.

Kati yao hakukuwa na mchezaji mwenye asili ya kucheza pembeni.

Wote walijaa katikati wakatoa ruhusa kwa Hassan Kessy na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kushambulia pembeni. Kama kawaida Simba walitawala soka kwa staili hii.

Licha ya Yanga kugundua janja hii ya Simba na kuamua kumwongeza Salum Telela katika kiungo, bado Simba walikuwa timu bora uwanjani hasa katika kipindi cha kwanza. Yanga walionekana kutetemeka.

Haji Mwinyi, mlinzi mtulivu na wa kisasa nchini hakuwa Haji Mwinyi tuliyemzoea. Naye aliingia katika orodha ya wachezaji waliokuwa wamemezwa na presha ya mchezo. Alikuwa anabutua tu.

Kwa kuwapanga Telela, Kamusoko na Haruna Niyonzima, Yanga walikuwa wameua kiaina winga moja ya kushoto na kubakiza tumaini pekee la mashambulizi upande wa kulia kwa Simon Msuva. Hata hivyo, Msuva alikuwa ovyo kama kawaida yake katika mechi za Simba.

Aliwekwa mfukoni na Tshabalala na akatulia. Hata alipotolewa mfukoni auchezee mpira alikuwa anafanya madudu. Dakika ya 34, Hans van der Pluijm akamwingiza Malimi Busungu ambaye alikuja kuibadili Yanga katika eneo la mbele kwa sababu walau yeye alitulia na mipira.

Wakati Simba wakicheza mpira mwingi katikati ya uwanja bila ya kutengeneza uhusiano wa uhakika na washambuliaji wake wa mbele, Mussa Mgosi na Hamis Kiiza, Yanga ilirudi katika staili yao ya zamani ya kucheza mipira mirefu na kukimbizana.

Ndipo walipowashtukiza Simba kwa bao la nyoka, Amiss Tambwe, ambaye waliwahi kumfuga wenyewe kabla ya kumtupia nyumba ya jirani. Walitegemea nini zaidi? Bao lenyewe lilitengenezwa kwa staili ya Kiyanga.

Busungu aliumiliki mpira katika boksi akautoa nje ukapigwe krosi na Yondani. Ulipomfikia Donald Ngoma alijaribu kupika tiktak ya mkasi lakini mpira ulikataa na kumfikia Tambwe ambaye analijua sana lango.

Hakupiga moja kwa moja. Alimtoa Jurko Mursheed katika njia na kuuchota mpira kwa umaridadi katika nyavu za Simba. Mpira ulitua hatua 30 tu kutoka katika jukwaa la mashabiki wa Simba.

Kabla ya Simba hawajajiuliza, Israel Nkongo alipuliza filimbi yake na kuiweka mfukoni. Wanaume 22 wakaenda mapumzikoni. Kipindi cha pili nilitazamia Simba wangekuja na kasi. Lakini ilitazamiwa kuwa kasi yao ingepungua kadri dakika zinavyokwenda.

Ndiyo, katika kipindi cha kwanza Simba walionekana kuwa na nguvu na stamina kuliko Yanga. Kila mchezaji wa Yanga alipotumia nguvu kuupata mpira kutoka kwa Simba alichemsha. Hata hivyo, ni zaidi ya msimu wa tatu huu Simba wanapoteza kasi kadri mechi inavyokwenda mbele. Ndicho kilichotokea.

Yanga iliendelea kucheza soka la malengo na kujichunga huku wakipiga pasi chache kujaribu kufika langoni, Simba walitumia njia ndefu zaidi ya kupiga pasi nyingi na kujaribu kutengeneza bao la soka. Kwa kasi hii, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alichoka. Umri unaonekana kumtupa mkono.

Kocha wake aligundua akamwita nje na kumwingiza Ibrahim Ajib lakini haikusaidia.

Dakika za mwisho za dakika 45 hizi za pili, Yanga walifanya kama zile za kwanza. Waliwanyemelea Simba na kufunga bao la Kiyangayanga.

Mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite ulimparaza mlinzi mmoja wa Simba ukatua kwa Malimi Busungu nyuma kabisa ya lango. Alikuwa amejipanga kuwa mpira ukitua maeneo hayo ni halali yake.

Wakati Busungu akipewa kadi ya njano na mwamuzi Israel Nkongo kwa kuvua jezi yake wakati anashangilia, kundi kubwa la mashabiki wa Simba lilikuwa liko nje likitafuta daladala za kurudi nyumbani.

Wakati Mbuyu Twite akipewa kadi nyekundu kwa kuchelewesha muda, jukwaa la Simba lilikuwa kama vile ni la mashabiki wa Coastal Union waliosafiri kutoka Tanga kuitazama timu yao ikicheza na Yanga.

Walibaki mashabiki wachache. Mashabiki wachache wa Simba waliobaki uwanjani walipata fursa tu ya kutazama utumbo uliokuwa unafanywa na mshambuliaji wao mrefu wa kimataifa wa Senegal, Pape N’daw. Aliingizwa kama mpango B wa Simba kwamba kwa sababu yeye ni mrefu basi timu ipige mipira mirefu kwa ajili yake.

Cha kushangaza mipira ya juu ilikuwa inachezwa na Yondani na Cannavaro. Ubora wa N’daw ulikuwa wapi? Hakuwa mzuri juu wala chini. Wakati akifanya utumbo huo, kilomita 10 kutoka Uwanja wa Taifa, Elius Maguli alikuwa akiifungia timu yake ya mkopo Stand United bao la ushindi dhidi ya JKT Uwanja wa Karume. Bao la tatu kwake ndani ya mechi mbili za Stand.

Wakati Israel Nkongo akimaliza dakika 100 za mechi yake, ambazo ni halali kwa sababu wachezaji wa Yanga wakiongozwa na Barthez walikuwa wanapoteza muda bila ya sababu za msingi, kulikuwa na mashabiki wachache waliokuwa wamesimama jukwaa la Simba.

Mkondo wa historia ulikuwa umegeuzwa. Hata hivyo, iliumiza zaidi mashabiki wa Simba kwa sababu timu yao ilicheza mpira haswa.

Yanga waliwafundisha tu jinsi ya kutumia makosa na jinsi ambavyo wana safu kali ya ushambuliaji nchini.

Mpaka watakapokutana tena Desemba 12 katika uwanja huu huu wa Wachina pambano la Nani Mtani Jembe, kwa sasa Yanga watakuwa wanaruhusiwa kutoa maneno machafu mtaani. Walau wametoka kifungoni.