Prime
Simba hii malizana nao mapema

TIMU ya Simba ukitaka kuibana, basi hakikisha unamalizana nayo ndani ya dakika ya dakika 45 za kwanza za mchezo husika kwani bila hivyo sahau kupata ushindi dhidi yao.
Simba imecheza mechi sita za mashindano, lakini katika mechi hizo michezo miwili ya Ngao ya Jamii haijafunga bao lolote.
Timu hiyo katika michezo minne imecheza mitatu Ligi Kuu na mmoja wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi hizo imeonyesha kutoruhusu mabao mengi kipindi cha pili ikiruhusu bao moja tu katika mchezo dhidi ya Power Dynamos uliomalizika kwa sare 2-2.
Simba irihusu bao hilo dakika ya 74 huku lile la kwanza likifungwa kipindi cha kwanza dakika ya 28.
Bao hilo la kipindi cha pili ndilo pekee ambalo Simba imeruhusu hadi sasa na ikionyesha ni wazi haina cha kupoteza muda huo ukifika.
Katika kipindi cha kwanza timu hiyo iliruhusu mabao matatu - mawili katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar katika dakika ya 20 na 22 yakifungwa na Matheo Anthony na lingine ni la mchezo dhidi ya Dynamos dakika ya 28.
Wakati Simba ikiwa ni ngumu kufungwa kipindi cha pili, yenyewe imeonyesha ubora wa kufunga muda wowote.
Simba katika kipindi cha kwanza imefunga mabao saba - matatu yakiwa katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar dakika za 5, 9 na 45, mchezo dhidi ya Dodoma Jiji dakika ya 44 na mechi dhidi ya Coastal Union dakika za 7, 11 na 40. Wakati huohuo katika kipindi cha pili Simba imefunga mabao manne - moja dhidi ya Mtibwa Sugar dakika ya 81, mchezo dhidi ya Power Dynamos dakika ya 59 na 90 na bao moja kwenye mechi dhidi ya Dodoma Jiji katika dakika ya 55.
Kocha mkuu wa Simba, Roberto OIiveira ‘Robertinho’ mara kwa mara amekuwa akisema silaha yake kubwa katika kikosi ni kuumiliki mpira.
Robertinho alikaririwa na gazeti hili akisema anapenda wachezaji wake wawe wanacheza soka la kumiliki mpira na kucheza pasi nyingi kwani inakuwa vigumu kwa wapinzani wao kuwafunga.
“Ukiwa na mpira ni ngumu kufanya makosa na kuruhusu kufungwa. Kwa hiyo ninavutiwa na namna ambavyo wachezaji wangu wanavyocheza ninavyotaka mimi,” alisema Robertinho.