Simba, Chama wamalizana kikubwa

Klabu ya Simba umetangaza msamaha kwa kiungo Mzambia, Clatous Chama ambaye aliadhibiwa Desemba 21, 2023 kutokana na utovu wa nidhamu.
Taarifa hiyo ilitolewa leo na Afisa Mtendaji Mkuu, Imani Kajula ikieleza kumsamehe mchezaji huyo baada ya kuwa nje kwa siku 40.
Chama ambaye msimu huu amefunga mabao mawili Ligi Kuu Bara amekuwa kwenye kiwango cha kupanda na kushuka tangu uwepo wa aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho Mbrazili, Roberto Oliveira 'Robertinho' na hadi sasa Mualgeria, Abdelhak Benchikha.
Katika taarifa hiyo uongozi wa Simba umesema “Hatua hii imetokana na maamuzi ya kamati ya ufundi ya Bodi ya Simba ambayo ilipitia barua ya maelezo ya Chama na uamuzi wa Kocha Benchikha wa kumsamehe kiungo huyo, hivyo kamati ya ufundi ya bodi ya hiyo ikaridhia kumsamehe na kusitisha kumfikisha kwenye kamati ya maadili ya klabu hiyo.”
“Chama anaungana na kikosi cha Simba kilicho mkoani Kigoma kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho Februari 3 katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
“Klabu ya Simba itaendelea kutilia mkazo ustawi wa nidhamu kama nguzo muhimu ya kujenga timu imara. Nidhamu ni moja ya tunu za klabu ya Simba.”