Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SIRI IMEFICHUKA! Hiki hapa kinachoipa jeuri Yanga kususia 'Dabi'

Muktasari:

  • Mchezo huo haukufanyika katika tarehe ya mwanzo baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya Simba kulalamika kuwa walizuiwa na watu wanadhaniwa kuwa walinzi wa Yanga.

Jumatatu, Mei 5 mwaka huu, kamati ya utendaji ya Yanga ilitoa tamko zito la kugomea kucheza mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu dhidi ya mtani wao wa jadi Simba ‘Kariakoo Dabi’ ambayo awali ilikuwa ichezwe Machi 8 mwaka huu.

Mchezo huo haukufanyika katika tarehe ya mwanzo baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) baada ya Simba kulalamika kuwa walizuiwa na watu wanadhaniwa kuwa walinzi wa Yanga.

Baada ya uamuzi huo, Yanga ilifungua shauri katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa michezo (CAS) lakini likatupwa kwa vile halikuanzia katika mamlaka za ndani ndipo Yanga ikaibuka na uamuzi huo wa kutocheza mechi hiyo ambayo tayari TPLB imepanga ichezwe Juni 15, 2025.

Katika taarifa yake ya kugomea kucheza mechi hiyo, Yanga imetaja kuwa ni kutokuwa na imani na mamlaka za ndani za uendeshaji soka ikidai inafanyiwa hujuma.

"Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuutaarifu Umma kuwa umepokea majibu kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kuhusu kesi yetu namba CAs 2025/A/11298.

"CAS imeielekeza Young Africans Sports Club kurudi kwanza kwenye kamati za ndani za soka ili kushughulikia kesi yetu kabla ya kurudi kwao kwa ajili ya hatua za rufaa.

"Lakini kutokana na uonevu, uvunjwaji mkubwa wa kanuni na upendeleo wa dhahiri kwa baadhi ya timu unaoendelea kufanywa na Mamlaka za soka Tanzania, Uongozi wa Young Africans Sports Club hauna imani na hauko tayari kupeleka shauri hilo kwenye mamlaka ambazo zinatenda dhulma," ilifafanua taarifa ya Yanga.

Yanga kupitia taarifa hiyo ikaweza msisitizo wa uamuzi kuhusu Kariakoo Dabi

"Aidha, Uongozi wa Young Africans Sports Club unapenda kuujulisha umma kuwa, msimamo wa klabu yetu juu ya mchezo namba 184 wa ligi kuu msimu huu uko palepale kuwa hatutashiriki kwenye mchezo huo kwa namna yoyote ile.

"Wanayanga wote, watakuwa tayari kuipambania haki kivyoyote vile ili kukomesha dhulma na uvunjwaji mkubwa wa kikanuni unaoendelea kufanywa na mamlaka za soka kwa maslahi mapana ya maendeleo ya soka nchini," ilisisitiza taarifa hiyo.

Muda mfupi baada ya Yanga, kutoa taarifa ya kugomea mechi, TPLB ilianika mabadiliko ya ratiba ambayo imeyafanya ikiwemo kuupangia tarehe mchezo huo na mingine ambayo haijachezwa.

Katika hali ya kawaida, hadi timu inafikia hatua ya kusisitiza zaidi ya mara tatu kugomea mechi, hapana shaka inakuwa na sababu ambazo zinaipa nguvu ya kuzibishia mamlaka za soka na hilo ndilo linaonekana kwa Yanga.

Kuna sababu tatu zinazoonekana zinaipa Yanga jeuri ya kutangaza na kusisitiza kuwa haitocheza mechi ya marudiano ya ligi kuu msimu huu dhidi ya Simba.


Udhaifu wa kikanuni

Kuna mambo mawili ya kikanuni msimu huu ambayo yanaipa nguvu na uhalali Yanga wa kugomea mechi.

Moja ni kwamba hakuna kanuni ambayo inalazimisha mchezo uahirishwe ikiwa timu moja imefanyiwa vurugu bali iliyopo inataja faini ya fedha hivyo Yanga pengine inaamini ndicho kilipaswa kufanywa na bodi ya ligi badala ya kuahirisha mechi.

"TFF/TPLB itachukua hatua kwa ukiukwaji wowote wa taratibu za mchezo kama zilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17 kwa kutoa onyo kali au karipio au kutoza faini kuanzia shilingi 1 milioni, mpaka shilingi 2 milioni  na/au kufungia michezo isiyozidi mitatu (3) au kipindi kisichozidi miezi mitatu (3). Faini kwa makosa yanayojirudia itatozwa kati ya shilingi 5 milioni na shilingi 10 milioni kwa mchezaji, kiongozi au timu," inafafanua ibara ya 62 ya kanuni ya 17 ya Ligi Kuu inayohusu taratibu za mchezo.

Jambo la pili ni kanuni kuipa uhakika Yanga kusalia kwenye ligi hata ikiadhibiwa kwa kutofika uwanjani tofauti na zamani ambapo adhabu ilikuwa ni kushushwa madaraja mawili.

Mfano timu ya Kimondo katika msimu wa 2016/2017 iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza wakati huo ilishushwa kwa madaraja mawili baada ya kushindwa kucheza mechi moja dhidi ya JKT Mlale ambayo ilipangwa kuchezwa Januari 28, 2017.

Kwa msimu huu, timu isipotokea uwanjani kwa mechi moja, inakatwa pointi 15 tu, adhabu ambayo inaenda sambamba na faini.

"Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF/TPLB na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo: Kutozwa faini ya sh5 milioni ambapo sh2.5 milioni itachukuliwa na bodi ya Ligi Kuu na sh2.5 milioni italipwa kwa timu pinzani.

"Kulipa fidia ya maandalizi/uharibifu wowote unaoweza kujitokeza. Kupokwa alama 15 (kumi na tano) katika msimamo wa Ligi na viongozi waliosababisha jambo hilo watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu. Endapo timu itakuwa na alama pungufu ya 15, itakuwa na alama hasi kwa kiasi kinachopungua kwenye msimamo wa ligi.

"Endapo timu itamaliza msimu wa Ligi ikiwa na alama hasi, itaanza na alama hizo hasi katika msimamo wa Ligi kwenye msimu unaofuata wa ligi ya hadhi yake," inafafanua kanun ya 31 ya Ligi Kuu msimu huu.


Uhakika kimataifa

Kama Yanga itashinda mechi tatu zijazo itakuwa na pointi 79 bila mechi na Simba, hivyo kama itafutiwa pointi 15 kwa kukacha mechi na Simba itamaliza ligi na pointi 64, ambapo Azam itamaliza na pointi 63 na Singida Black Stars pointi 62 kama zitashinda mechi zao zilibaki.

Hivyo moja kwa moja Yanga itabaki nafasi ya pili nyuma ya Simba na kuwa imefuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.

 Bado Yanga itakuwa na nafasi ya kujiuliza kwa Simba kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kama zote zitafuzu.


Kinga ya vyombo vya usalama

Mambo mawili yalitajwa na TPLB kama sababu ya kuahirishwa kwa mechi hiyo ambayo ni viashiria vya uvunjifu wa amani na pia vya rushwa.

Hata hivyo, sio Jeshi la Polisi ambalo lina mamlaka ya kulinda usalama wa raia na mali zao wala Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ambazo zimethibitisha tuhuma hizo.

Vyombo hivyo visipothibitisha hilo, maana yake madai ya TPLB yatapoteza uhalali na hapo Yanga itakuwa na nguvu mbele za umma.