Simba akili mingi, waja na mikakati mizito, kwenda Sudan leo

SIMBA wamerejea mazoezini jana lakini wamecheza akili mingi ili kuganda kileleni mwa msimamo wa ligi na kukanyaga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kikosi hicho kitaondoka nchini leo Alhamisi kwenda Sudan kucheza mechi mbili za kirafiki za maana. Watacheza dhidi ya Asante Kotoko Agosti 28 kabla ya kuwavaa Al Hilal Agosti 31. Wakirudi Dar es Salaam watakipiga na AS Arta Solar ya Djibout iliyoko Jijini. Simba itakwea na wachezaji wasiopungua 20 huku ikiwakosa tisa waliopo timu ya Taifa na baadhi walioomba udhuru kwenda kwao nje ya nchi.
Kocha wa Simba, Zoran Maki alisema mechi hizo za mashindano maalum yaliyoandaliwa na Al Hilal ya Sudan, zitawasaidia kwani kuna utofauti wa kiufundi kucheza mashindano hayo na kama wachezaji wake waliobaki wangeendelea kufanya mazoezi na kucheza mechi zile za ndani.
Alisema kwanza utimamu na ufiti wa wachezaji utakuwa juu kwani bado watakuwa wapo katika mashindano, timu itaendelea kuwa kwenye ushindani, mechi hizo mbili zitaonyesha taswira ya timu maeneo gani wapo vizuri na kwenye mapungufu ili kurekebisha kabla ya kuingia kwenye michuano ya kimataifa.
Simba wataanzia hatua ya awali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakicheza na Nyanza Bullets ya Malawi ugenini Septemba 10.
“Sitakuwa na wachezaji wote ila naamini wale waliopo kwenye timu ya taifa wanapata mazoezi ya kutosha na ushindani katika mechi hizo mbili na wakirudi watakuwa levo moja ya utimamu wa mwili na hali ya ushindani kama hao nitakaokuwa nao Sudan,” alisema Zoran.
“Pia Simba tunaenda kucheza mechi za kimataifa na aina ya timu, ushindani ambao tutakutana nao ni kama wa kule Sudan dhidi ya Asante Kotoko na Al Hilal kwahiyo ni faida kubwa kwetu haya mashindano kabla ya kucheza na Nyasa Big Bullet katika mchezo wa kwanza Ligi ya mabingwa Afrika msimu huu,”
“Naifahamu Al Hilal nimewafundisha kabla ya kuja Simba watatupa ushindani na presha ile kama tunacheza ugenini na kuanza kuzoea hali hiyo kabla ya kwenda Malawi katika mechi ya Nyasa au nchi nyingine katika hatua zinafuata.
“Kwenye mechi tatu za mashindano ambazo tumecheza kuna mabadiliko ya baadhi maeneo kulingana na maingizo mapya kwenye timu kule Sudan tunaendelea kufanya hivyo na nadhani baada ya muda mfupi kila kitu kitakuwa sawa na mabadiliko hayo hayatakuwa mfululizo.”
Katika hatua nyingine Zoran alisema Simba inahitaji kufanya vizuri katika mashindano ya ndani na anapambana kuhakikisha kikosi kinakuwa na makali zaidi ya michezo miwili iliyopita. Ofisa Mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema: “Kualikwa na Al Hilal ni moja ya mafanikio ya ushirikiano wetu pamoja na klabu mbalimbali Afrika, haya ni matunda ya mahusiano yaliyojengwa kwenye michuano ya Simba Super Cup 2021.”