Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku 50 za usajili zilizotikisa vigogo

Klabu inayoendeshwa kisomi nchini ya Azam, ilifanya usajili wake mapema na kwa mahitaji maalumu ambapo imewasajili nyota wanne pekee wapya na kuwatoa watatu kwa mkopo.

Muktasari:

Kila timu ilikuwa ikifanya yake kuhakikisha mambo yanaenda sawa kabla ya dirisha hilo kufungwa.

DIRISHA la Usajili barani Ulaya linahitimishwa usiku wa saa sita leo Jumanne.

Kwa upande wa Tanzania Bara kulikuwa na siku 50 zilizotetemesha vigogo vya soka nchini katika zoezi kama hilo lililofunguliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kuanzia Juni 15 hadi Agosti 6.

Klabu za Simba, Yanga na Azam zilikuwa zikipigana vikumbo kukimbizana na muda wa usajili wa awali ambapo zilisajili kisha zikakausha kama vile zilishamaliza kazi.

TFF ikaziangalia na kuona kama zilikuwa bado hazijakaa vema na kuziongezea tena wiki mbili hadi Agosti 20 nazo zikachangamkia siku hizo fasta kwa kusajili wachezaji kadhaa kisha zikauchuna tena kana kwamba zilishamaliza usajili wao.

TFF ikaziangalia tena kwa jicho pana na kujiridhisha kuwa zilizikuwa bado hazijamaliza mambo na kuongeza siku nyingine 10.

TFF iliongeza siku hizo 10 ambazo kama klabu zingekuwa zinasajili basi zingepaswa kulipa na faini ya Sh500,000 na kutamka wazi kwanza zoezi lingemalizika usiku wa juzi Jumapili na hapa ndipo vikumbo vya usajili wa lala salama vilipoanza.

Kila timu ilikuwa ikifanya yake kuhakikisha mambo yanaenda sawa kabla ya dirisha hilo kufungwa.

Juzi Jumapili saa 6:00 usiku, dirisha hilo la usajili kwa klabu za Ligi Kuu na zile za Ligi Daraja la Kwanza lilifungwa ambapo Yanga na Simba zilifanya maamuzi magumu ili kuendana na siku hiyo ya mwisho ya usajili licha ya kuwa na muda mrefu wa maamuzi hapo nyuma.

Simba ilimsainisha straika ngongoti, Pape N’daw kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr kuridhishwa na uwezo wake ambapo Yanga wao waliutumia muda huo kuvunja mkataba na beki Mghana, Joseph Zuttah.

Balaa la Simba

Simba haikuishiwa vituko katika usajili wa msimu huu baada ya viongozi wa timu hiyo kuanza kukimbizana masaa machache kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo la usajili na kusahau kabisa kuwa dirisha lilikuwa wazi tangu mwezi Juni.

Harakati kubwa za Simba hiyo juzi zilikuwa ni kumpata straika mmoja wa uhakika ambapo katika rada zao walikuwa na Kevin Ndayisenga, Pape N’daw na Makan Dembele, lakini mwishowe ilimsainisha Msenegali N’daw pekee.

Ndayisenga ambaye alikuwa na nafasi kubwa zaidi aliachwa kutokana na dau lake kuwa kubwa ambapo dili lake lote lilihitaji zaidi ya dola 55,000 (Sh110 milioni), fedha ambazo Simba iliziona nyingi mno na hawakuwa tayari kuzitoa, huku Dembele akiachwa kutokana na kususia majaribio.

Katika hali ya kushangaza, Simba ilionekana kuhaha kutaka kumsainisha kipa wa JKU ya Zanzibar, Abdulrahman Mohamed, katika dakika za mwishoni wakati kipa huyo alishaitwa Dar es Salaam mara mbili na mabosi wa timu hiyo na kuishia kumpiga kalenda.

Hata hivyo licha ya kukubaliwa kuondoka na timu yake ya JKU, Simba ilishindwa kuwasilisha fedha ilizotakiwa na kutaka kumsainisha kwa ahadi jambo ambalo liligomewa na timu hiyo hivyo kumkosa kipa huyo.

Kwa ujumla Simba imewasajili Vincent Angban, Emiry Nimubona, Samir Haji Nuhu, Mohamed Faki, Justice Majabvi, Peter Mwalyanzi, Emmanuel Mtumbuka, Hamis Kiiza, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Pape N’daw, Danny Lyanga na kinda Boniface Maganga.

Yanga

Mabingwa wa soka nchini, Yanga ilifanya usajili wake mapema kabla ya dirisha kufungwa lakini ilipata nafasi dakika za mwishoni ya kuachana jumla na beki Mghana, Joseph Zuttah ambaye alishindwa kuivutia timu hiyo licha ya kumsajili mwezi Julai.

Usajili mwingi wa Yanga ulifanyika mapema ambapo iliwanasa Malimi Busungu, Deus Kaseke, Geofrey Mwashiuya, Benedict Tinoco, Donald Ngoma na Haji Mwinyi Mngwali.

Baadaye timu hiyo ilihaha kukamilisha usajili wake kabla ya kufungwa kwa dirisha ambapo awali ilikuwa Agosti 6 hivyo kumsainisha Thabani Kamusoko kutoka FC Platinum ya Zimbabwe kama ilivyo kwa Ngoma. Baada ya kuongezwa kwa wiki mbili klabu hiyo ilifanya usajili wa kipa Mudathir Khamis, beki Mtogo Vincent Bossou na mshambuliaji Matteo Saimon na kukamilisha usajili wake mapema kabla ya Agosti 20.

Azam

Klabu inayoendeshwa kisomi nchini ya Azam, ilifanya usajili wake mapema na kwa mahitaji maalumu ambapo imewasajili nyota wanne pekee wapya na kuwatoa watatu kwa mkopo.

Azam imewasainisha Allan Wanga kutoka Kenya ambaye alikuwa akicheza El Merreikh ya Sudan, Jean Mugiraneza ‘Migi’ kutoka APR ya Rwanda, Ramadhan Singano ‘Messi’ kutoka Simba na Ame Ali kutoka Mtibwa Sugar.

Hata hivyo Azam ilitaka kuutumia muda wa dakika za mwishoni kusajili nyota mpya na kuachana na winga Brian Majwega, lakini dili hilo lilishindikana hivyo kusubiri hadi wakati wa usajili wa dirisha dogo, pia iliwatoa wachezaji wake kadhaa kwa mkopo katika klabu nyingine akiwamo Jospeh Kimwaga aliyetua Msimbazi na chipukizi wawili waliotua Majimaji Songea.

Kerr aomba wiki mbili

Katika hatua nyingine kocha wa Simba, Dylan Kerr ameomba muda wa wiki mbili ili kupandisha makali ya N’daw kwa madai kuwa licha ya kwamba wamemsainisha bado hayuko fiti vilivyo kufanya makubwa pale Msimbazi.

Kerr alisema endapo N’daw ataweka akili katika mazoezi, ndani ya wiki mbili ataanza kufanya kazi ya maana huku pia akidai anavutiwa naye zaidi kutokana na kuwa na umri mdogo.

“Tumemsajili lakini bado hayupo fiti vilivyo, anaonekana kuwa mchezaji mzuri na atatuongezea wigo katika nafasi ya ushambuliaji, lakini anahitaji kufanya mazoezi makali kwa wiki hizi mbili,” alisema kocha hiyo Mwingereza.