Siasa, wafadhili vimeua soka Zanzibar-3

Muktasari:
Katibu Mkuu wa JKU, Saadu Ujudi anasema: “Hatuna bajeti ya usajili, huwa tunasajili kutokana na mahitaji ya kocha, lakini kwetu mchezaji ghali hazidi ni Sh1 milioni na kwa vile ni timu ya jeshi na kama tumemtoa uraiani huwa tunampa posho, hakuna mshahara.”
KATIKA toleo lililopita tuliona jinsi malipo madogo ya usajili kwa wachezaji na kiingilio kidogo kuwa ni kati ya mambo yanayokwamisha soka la Zanzibar. Sasa endelea…
Katibu Mkuu wa JKU, Saadu Ujudi anasema: “Hatuna bajeti ya usajili, huwa tunasajili kutokana na mahitaji ya kocha, lakini kwetu mchezaji ghali hazidi ni Sh1 milioni na kwa vile ni timu ya jeshi na kama tumemtoa uraiani huwa tunampa posho, hakuna mshahara.”
Miaka ya nyuma timu za uraiani ndizo zilizokuwa zinatoa huduma bora kwa wachezaji na kuwalipa vizuri, lakini mambo yamegeuka, mchezaji anayecheza uraiani akisajiliwa na kupewa fedha ya usajili, huo unakuwa mwisho wake hata akiumia anatakiwa ajihudumie mwenyewe.
Hali ni tofauti na timu za majeshi, wakisajili mchezaji ambaye si mwanajeshi hupewa fedha ya usajili, hana mshahara, anapewa posho tu na akiumia anapata huduma za matibabu.
Wachezaji wa kigeni
Zanzibar wametoa wachezaji wengi wazuri waliowahi kucheza na wanaocheza Ligi Kuu Bara baadhi yao ni Nadir Haroub ‘Canavaro’ (Yanga), Abdi Kassim aliyezichezea Yanga na Azam, Agrey Moris (Azam), Ame Ally (Mtibwa Sugar), Ally Badru, Abdul Makame na Awadh Juma (Simba), Said Morad, Hamis Mcha, Muhidin Ally na Mudathir Yahya (Azam), Mohamed Faki (JKT Ruvu), Abdulhalim Humud (Coastal Union) na Suleiman Kassim (Polisi Moro).
Cha kusikitisha ukiacha miaka ya nyuma ambayo Malindi, Small Simba na timu nyingine zilizotamba na wachezaji wa kigeni hasa kutoka Bara, kwa sasa hakuna mwamko huo ingawa kuna timu zimesajili wachezaji kutoka Bara ambao hawana majina makubwa na usajili wao pia ni wa bei chee.
Viwanja kuvamiwa, kutelekezwa
Zanzibar kuna viwanja ambavyo hutumiwa na timu mbalimbali ingawa mechi za Ligi Kuu zote huchezwa Uwanja wa Amaan, Unguja na Gombani, Pemba, uvamizi wa viwanja si mkubwa sana visiwani humo zaidi ya viwanja ambavyo vilikuwa eneo la Amaan na watu walifanya makazi yao mpaka sasa.
Kuna uwanja maarufu ambao ni wa kwanza kujengwa visiwani Unguja chini ya utawala wa hayati Abeid Amaan Karume, Uwanja wa Mao, kwa sasa unaelekea kuwa kichaka au pori, hautumiwi kwa mechi za Ligi Kuu, hutumiwa na timu za ligi za chini huku jukwaa kuu na sehemu za kukaa mashabiki vikiwa vimechakaa na hakuna anayekumbuka kuukarabati uwanja huo ili walau Unguja kuwe na viwanja viwili.
ZFA
Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) ndio wasimamizi wa soka Zanzibar, ndio wanaosimamia ligi zote na timu ya Taifa. ZFA wana mawazo tofauti kuhusu soka la Zanzibar wakilinganisha hali ilivyo sasa na miaka ya nyuma.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya ZFA, Ally Bakari anasema: “Miaka ya nyuma soka lilionekana kupanda kwa sababu baadhi ya timu zilikuwa na wafadhili, ndiyo maana ushindani ulikuwepo lakini ukiangalia kwa umakini kipindi hiki soka limepanda sana visiwani hapa.
“Hiyo ni kwa sababu kuna mdhamini tofauti na miaka ya nyuma na ZFA haikuwa na udhamini ingawa timu zilikuwa na wafadhili wao na hata zile ambazo hazikuwa na wafadhili walijitoa kudhihirisha ubora wao kwa timu zenye wahisani.
“Zamani pia, wachezaji wengi walitoka Bara kuja kucheza hapa na sasa wanatoka Zanzibar kwenda Bara, hiyo pia inaonyesha ni kiasi gani hapa kuna vipaji kwa vijana ukilinganisha na miaka hiyo, yote hayo yanatokana na ushindani uliopo, kwani hata kanuni za usajili zimebadilika, zamani ilikuwa ni wachezaji watano kutoka Bara na sasa ni wanane na wote wanaruhusiwa kucheza kwa wakati mmoja.
“Changamoto kubwa ipo kwenye udhamini ingawa tunao Grand Malta ambao pia huu ni mwaka wao wa mwisho kudhamini ligi yetu na hatujajua kama wataendelea, lakini tunataka kuongeza idadi ya timu kutoka 12 hadi 16 ili vijana wetu waweze kucheza kwani hawapati fursa ya kuonyesha vipaji vyao kutokana na uchache wa timu kwenye ligi,” anasema Bakari.
Bakari pia anafafanua maendeleo ya soka visiwani humo kwa upande wa viwanja, anasema uwanja mkongwe wa Mao ambao ni kama umetelekezwa, wana mipango ya kuujenga kwa msaada wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Japokuwa ZFA imepitisha wazo la kuongeza timu za Ligi Kuu, lakini timu 12 zilizopo kwenye ligi hiyo zinalalamika juu ya udhamini mdogo wa Grand Malt kwamba haukidhi mahitaji ya timu, hivyo ZFA inawezekana inajitwisha mzigo mwingine au inazitwisha timu mzigo ambao hawawezi kuubeba kwani kuandaa timu kwa mechi za ligi kunahitaji fedha nyingi.
Lunyamila
Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Edibily Lunyamila ni miongoni mwa wachezaji waliocheza Ligi ya Zanzibar, aliichezea Malindi wakati huo inafadhiliwa na Noushad, kwa upande wake anasema:
“Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba, siasa za vyama vingi liliua soka la Zanzibar, mfadhili wetu alijitoa baada ya Jimbo la Malindi kuchukuliwa na CUF na baada ya hapo tuliambiwa wazi kwamba timu haiwezi kuendelea ndiyo maana tuliamua kurudi Bara. Lakini Zanzibar ni kisiwa ambacho kina wachezaji wengi wenye vipaji mpaka sasa, hilo halina ubishi.
“Wafadhili wanatakiwa kurudi kuzisaidia timu za Zanzibar kama ilivyokuwa zamani wakati Malindi, Shangani na Mlandege zilipokuwa na ufadhili ingawa Small Simba hawakuwa na mdhamini lakini walifanya vizuri kutokana na ushirikiano uliokuwepo baina ya viongozi wenyewe wa timu.
“Ligi pia ilikuwa na ushindani kwa sababu kulikuwa na mwingiliano wa wachezaji kutoka sehemu mbalimbali duniani, kwetu walikuwepo waliotoka Zambia na Bulgaria, pia kulikuwa na Kombe la Muungano, tulikuwa tunakutana na Simba na Yanga ambazo kwa wakati huo, pia zilikuwa na wadhamini,” anasema na kuongeza.
“Kingine kilichoshusha soka Zanzibar ni kukataa udhamini wa kilevi, serikali na ZFA wanatakiwa kuangalia upya mfumo wa udhamini wa ligi yao,” anasema Lunyamila.
Noushad Mohamed
Norshad alikuwa ni mfadhili wa timu ya Malindi lakini inaelezwa baada ya mfumo wa vyama vingi kuingia nchini na Jimbo la Malindi kuchukuliwa na CUF, aliamua kuachana na mipango yake yote ya kuisadia Malindi kwa madai kwamba wananchi wa jimbo hilo wamekisaliti chama tawala.
Juhudi za kumsaka Noushad ziliendelea lakini bado hakuwa tayari kuzungumzia soka la Zanzibar. Mwisho