Serengeti kujipima na Arusha Utd, Polisi Tanzania

Muktasari:
Hata hivyo kocha mkuu wa timu hiyo, Oscar Milambo aliliambia Mwanaspoti michezo hiyo itawapa motisha wachezaji wake na kupata utimamu wa mwili.
KIKOSI cha timu ya Taifa Tanzania chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kinacheza mchezo wa kujipima nguvu leo jioni dhidi ya Arusha Utd, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Serengeti wameweka kambi Arusha wakiwa wanajiandaa kwenda nchini Uturuki kwenye Mashindano ya UEFA Assist mwishoni mwa mwezi huu.
Ikiwa inaendelea na kambi hiyo tayari imeshapokea mialiko miwili ya kucheza michezo ya kirafiki dhidi ya Arusha Utd ambayo inatokea jijini hapo na kushiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Baada ya mchezo huo Serengeti watashuka tena dimbani Jumatatu kukipiga na Polisi Tz ambayo nayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Hata hivyo kocha mkuu wa timu hiyo, Oscar Milambo aliliambia Mwanaspoti michezo hiyo itawapa motisha wachezaji wake na kupata utimamu wa mwili.
“Ni mechi nzuri na ni ya kirafiki katika kikosi changu kuna aina ya soka ambalo nalihitaji na ninaamini kabisa kwamba nitalipatia picha katika michezo hii,” alisema.