Senzo: Yanga imeimarika

YANGA imesema kwa sasa wanasubiri majibu ya vikao kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lakini liwe liwalo lazima waishinde Namungo FC katika mchezo wa Jumamosi.

Yanga ilitarajia kuondoka leo kuwafuata Namungo huko Lindi katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara na kwa kauli ya Mshauri wa masuala ya uongozi, Senzo Mazingisa, Kocha Nesreddine Nabi amegundua jinsi ya kuwatumia mastaa wake kupata matokeo ya kufurahisha.

Senzo aliongeza kuwa mzuka mkubwa katika kikosi chao ni hatua ya maboresho wanayoendelea kuyapata wachezaji wao kupitia kocha wao mpya Nabi.

“Timu imeanza kuimarika sana, ni bahati mbaya mchezo wa Simba umeahirishwa, lakini wanachama na mashabiki wangeona kitu tofauti kutoka kwa kocha wetu, wachezaji wameanza kumwelewa kwa kiasi kikubwa,” alisema Senzo.

“Mechi na Namungo haitakuwa rahisi, lakini kwa sasa tuna kikosi ambacho ukiongeza mbinu za kocha mashabiki wetu watakuja kuona kitu tofauti katika kuongezeka kwa ubora wa mbinu.

“Mashabiki wetu warudishe akili yao kwa timu yao, hili ndilo muhimu kwa sasa, waachane kwa muda na masuala ya mchezo uliopita, ni muhimu kuendelea kushinda mechi zijazo.”

Kuhusu mechi ya juzi, Senzo ameliambia Mwanaspoti kuwa kupitia mwongozo wa Waziri Mkuu, Majaliwa wao kama Yanga wanasubiri kusikia kipi kitaamuliwa, lakini akili yao yote imehamia Namungo.

“Huku Yanga tunachosubiri ni kipi kitaamuliwa kati ya serikali na TFF kama ambavyo Waziri Mkuu ameelekeza, uamuzi wa hapo ndio Yanga tutakuwa na kipi cha kuzungumza,” alisema.

Senzo ambaye ni raia wa Sauzi, alisema kwa sasa akili yao kubwa ni kuwafuata Namungo ili kuhakikisha wanaendeleza mzuka wa ushindi katika mechi zilizosalia.