Samatta amsomesha namba Ronaldo Ulaya

Muktasari:

  • Mohamed Salah ambaye aliiongoza Liverpool kuitandika Bournemouth kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England ana idadi sawa ya mabao na Cristiano Ronaldo kabla ya mchezo wa jana ambapo alikuwa na kibarua cha kuingoza Juventus dhidi ya ving’ang’anizi, Sassuolo.

WIKENDI imemalizika kibabe kwa nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ‘Samagoal’ kuwasomesha namba Cristiano Ronaldo, Luka Jovic, Kylian Mbappé na Mohamed Salah kwenye orodha ya wafungaji katika ligi mbalimbali barani Ulaya.

Baba lao kwenye orodha ya mastaa wanaofanya kweli kwenye ligi za barani humo ni Lionel Messi wa Barcelona ambaye kabla ya mchezo wa jana Jumapili usiku dhidi ya Athletic Bilbao alikuwa na mabao 21 kwenye La Liga ambayo ni Ligi Kuu Hispania.

Messi anafuatiwa na Msenegali, Mbaye Diagne wa Kasimpasa ya Uturuki mwenye mabao 20.

Anayeshika nafasi ya tatu barani humo katika zile ligi kubwa zenye ushindani ni Samagoal aliyetumbukiza kambani mabao 19, Ligi Kuu Ubelgiji ambayo ni maarufu kama Jupiler Pro.

Wenye mabao 18 ni Mbappé wa PSG ambaye ndiye kinara kwenye Ligi ya Ufaransa ‘Ligue One’ na Luuk de Jong ambaye ni mtambo wa mabao wa PSV Eindhoven anayewaburuza wenzake, Ligi Kuu Uholanzi ‘Dutch Eredivisie’.

Mohamed Salah ambaye aliiongoza Liverpool kuitandika Bournemouth kwa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu England ana idadi sawa ya mabao na Cristiano Ronaldo kabla ya mchezo wa jana ambapo alikuwa na kibarua cha kuingoza Juventus dhidi ya ving’ang’anizi, Sassuolo.

Upande wa mastaa wa Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’, wanaongozwa na Luka Jovic wa Frankfurt, ambao wamepitwa na Samagoal mabao matano, Jovic ana mabao 14 kwenye kilele cha wafungaji huku akifuatiwa na Robert Lewandowski wa Bayern Munich mwenye mabao 13.

Guillaume Hoarau wa BSC Young Boys ana mabao 13 Ligi Kuu Uswiss sawa na Dyego Sousa wa Braga ya Ureno, huku Jonatan Soriano wa RB Salzburg akiwa na mabao manane, Ligi Kuu Austria.

MOTO CHINI

Samagoal ni moto chini aiseeh!! Unaambiwa mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba, African Lyon za Tanzania na TP Mazembe ya DR Congo amehusika kwenye mabao 10 ya KRC Genk iliyoyapata katika michezo minane iliyopita ya Jupiler Pro.

Katika michezo hiyo ni dhidi ya Anderlecht, Kortrijk, KV Oostende, AS Eupen, Gent, Sint-Truiden, Royal Excel Mouscron, Waasland-Beveren na Standard Liège amefunga mabao manane na kutengeneza pasi moja ya bao.

MSIKIE MBONGO UBELGIJI

Shabiki namba moja wa Samagoal kule Ubeligi ambaye ni raia wa Tanzania, Jeff Megan alisema anatambua huu unaweza kuwa msimu wa mwisho kwa mshambuliaji huyo wa Kitanzania kucheza soka ubelgiji

“Samatta ni mtu mwingine Genk, ataondoka kwa heshima anapendwa na kila mtu. Siku hizi natembea kifua mbele mitaani, Wabelgiji wanatambua kuwa kuna taifa linaitwa Tanzania,” alisema Jeff.