Salum Kihimbwa aingia anga za Mashujaa

Muktasari:
- Nyota huyo amesimamishwa kwa muda usiojulikana baada ya kumpiga mwamuzi katika mechi ya kirafiki kati ya timu hiyo na Wapolo iliyochezwa Alhamisi ya Juni 12, 2025 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ilikoweka kambi.
WAKATI uongozi wa Fountain Gate, ukimsimamisha kiungo mshambuliaji wa kikosi hicho, Salum Kihimbwa kwa utovu wa nidhamu hadi pale itakapotoa taarifa nyingine, nyota huyo kwa sasa anawindwa na maafande wa Mashujaa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo amesimamishwa kwa muda usiojulikana baada ya kumpiga mwamuzi katika mechi ya kirafiki kati ya timu hiyo na Wapolo iliyochezwa Alhamisi ya Juni 12, 2025 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha ilikoweka kambi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau alisema wao kama viongozi wanazingatia nidhamu katika utendaji wao wa kazi hivyo, hawako tayari kuvumilia mchezaji yeyote akienda kinyume cha utaratibu ambao wamejipangia.
Sasa wakati hatua hiyo ikichukuliwa, taarifa zinaeleza uongozi wa kikosi hicho hauna mpango wa kumrejesha kikosini kutokana na matatizo ya kinidhamu, jambo linaloipa jeuri Mashujaa kuanza kuiwinda saini yake.
Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika alisema kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala la usajili, kwa sababu bado kuna mechi mbili zimebaki kumaliza msimu huu, hivyo baada ya Ligi Kuu Bara kuisha ndipo wataanza harakati hizo.
“Ni mapema sana ndugu yangu kuzungumzia hilo kwa sababu tunapigania kumaliza vizuri ili kujihakikishia kubaki Ligi Kuu Bara, kisha ndipo tutaanza upya mipango mikubwa ya kuboresha kikosi chetu,” alisema Meja Abdul.
Mwanaspoti linatambua, Kihimbwa mkataba alionao na Fountain unafikia tamati mwisho wa msimu huu, ingawa kuna kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi, japo viongozi wa kikosi hicho hawako tayari kuendelea kubaki na mchezaji huyo kwa msimu ujao.
Kihimbwa amewahi pia kutamba na timu mbalimbali kama Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji na Tanzania Prisons.