Clara sasa kufuatiliwa kwa teknolojia

Muktasari:
- Shirikisho hilo limepanga kuzikabidhi timu zote za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza fedha kwa ajili ya vifaa mbalimbali vya kiteknolojia ili kukuza soka la wanawake nchini humo.
NYOTA wa timu ya Taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’, Clara Luvanga na chama lake la Al Nassr kuanzia msimu ujao wataanza kutumia teknolojia mbalimbali kwenye michezo, kwa mujibu Shirikisho la Soka la Saudi Arabia (SAFF).
Shirikisho hilo limepanga kuzikabidhi timu zote za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza fedha kwa ajili ya vifaa mbalimbali vya kiteknolojia ili kukuza soka la wanawake nchini humo.
Vifaa hivyo ni pamoja na GPS ambacho kazi yake ni kufuatilia maendeleo ya mazoezi, utimamu wa mwili na kupunguza hatari ya majeraha.
Pia timu hizo kila moja itapewa udhamini pamoja na mchunguzi wa vipaji, daktari wa kutoa ripoti za afya na wataalamu wa lishe kwa ajili ya milo ya wachezaji
Makamu wa Rais wa SAFF, Lamia Bahaian alisema; “Tumeshuhudia maendeleo makubwa kwenye soka la wanawake katika mwaka uliopita. Ongezeko la ufadhili kwa msimu huu linaonyesha wazi dhamira yetu ya kuendeleza zaidi. Tunataka kutoa fursa zaidi kwa wanawake na kujenga msingi imara wa soka la wanawake nchini.”
Aliongeza ongezeko la nyota wa kigeni kwenye ligi hiyo akiwemo Clara limeongeza pato kubwa kwenye soka la wanawake.
Kama Clara ataendelea kusalia Saudia msimu ujao utakuwa msimu wake wa tatu tangu alipojiunga nao mwaka 2023 akitokea Dux Lugrono ya Hispania.
Msimu wa kwanza nyota huyo wa timu ya taifa ‘Twiga Stars’ alifunga mabao 13 na msimu huu kapachika wavuni mabao 19.