Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sakata la mchezo wa Dabi latinga bungeni, Serikali yajibu

Muktasari:

  • Kauli hiyo imekuja baada ya swali la nyongeza liloulizwa na Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga aliloliuliza leo Juni 11,2025 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Sakata la mchezo wa Dabi ya Kariakoo unaozikutanisha Yanga dhidi ya Simba, limeingia bungeni ambapo Serikali imesema haiwezi kuingilia kwa kuwa mchezo wa mpira wa miguu una kanuni zake kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo imekuja baada ya swali la nyongeza liloulizwa na Mbunge wa Makete (CCM), Festo Sanga aliloliuliza leo Juni 11,2025 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Sanga amesema kuimarisha timu ya Taifa ni pamoja na kuhakikisha sheria na taratibu za michezo zinafuatwa.

“Ligi yetu inaelekea mwisho lakini kumekuwa na mvutano wa hizi timu mbili (Yanga na Simba) na viongozi wa TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania), ipi kauli ya serikali?” Ameuliza Sanga.

Kabla ya Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kutoa kibali kwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma (MwanaFA) kujibu, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya alianza kuzungumza nje ya kipaza sauti.              

Kufuatia hatua hiyo, Dk Tulia alimhoji Bulaya kama anataka kumsaidia Naibu Waziri kujibu.

Hata hivyo, baadaye Spika alimpa nafasi MwanaFA  kujibu swali hilo ambapo alisema kama ambavyo wabunge wanafahamu shughuli za mchezo wa mpira wa miguu zina mamlaka zake za kitaifa na kimataifa.

“Na tumekuwa tukisisitiza mara kwa mara Serikali kutoingilia moja kwa moja uendeshaji wa shughuli hizo ili kuepuka kuja pengine hata kufungiwa na FIFA (Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa) katika nyakati hizi ambapo kitakwimu nchi yetu inafanya vizuri sana katika uendeshaji wa shughuli za mpira wa miguu,” amesema.

Amesema mamlaka za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za mpira wa miguu nchini ziko chini ya TFF sambamba na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TLPB).

Amesema Serikali hata taarifa ambazo wanazitoa bungeni huwa wanapata taarifa kutoka katika mamlaka hizo kuhusu mchezo huo.

“Tunafuatilia kwa ukaribu jinsi ambavyo mgogoro huu na unavyoendelea kutatuliwa, lakini huku tukijaribu kwa kiwango kikubwa kabisa kutoingilia moja kwa moja maamuzi ya TFF na Bodi ya Ligi,” amesema na kuongeza.

“Lakini tumekuwa tukifuatilia kwa karibu huku tukisisitiza TFF na Bodi ya Ligi kufuata na kutekeleza kanuni na sheria ambazo wamejiwekea.”

Amesema wanafanya hivyo kwa kuhakikisha hawaingilii moja kwa moja ili kuepuka nchi kufungiwa kwa vile mchezo wa mpira wa miguu unajiendesha wenyewe.

Baada ya kumaliza kujibu, Dk Tulia alimpa nafasi Bulaya aseme alichotaka kukisema ambapo amebainisha taratibu na sheria ni pamoja na kupata ripoti kwa nini mchezo wa Machi 8,2025 hawakucheza.

Kauli hiyo ilifanya Dk Tulia kumweleza Bulaya kwa kuwa yeye alikuwa akikataza ushabiki lakini leo anautaka ushabiki.

“Haya mbunge wa Simba anayetaka kumjibu,” amesema Dk Tulia ambapo alimruhusu Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko kumjibu Bulaya.

Matiko amesema kama alivyojibu naibu waziri lazima waheshimu kanuni ambazo zinaongoza mchezo wa mpira wa miguu ili waweze kukuza vipaji na wasiweke ushabiki.