Straika Coastal yamemtibukia Bara

Muktasari:
- Nyota huyo alipata majeraha hayo dhidi ya Singida Black Stars, ambao kikosi hicho cha Coastal Union kilishinda mabao 2-1, katika mechi ya Ligi Kuu baina ya miamba hiyo, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, Aprili 10, 2025.
MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Maabad Maulid huenda akakosa mechi zote mbili zilizosalia za kumaliza Ligi Kuu Bara msimu huu, kutokana na kutokuwa fiti kwa asilimia 100 kwa sasa, baada ya nyota huyo kujiumiza tena goti lake la mguu wa kulia.
Nyota huyo alipata majeraha hayo dhidi ya Singida Black Stars, ambao kikosi hicho cha Coastal Union kilishinda mabao 2-1, katika mechi ya Ligi Kuu baina ya miamba hiyo, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, Aprili 10, 2025.
Katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara ambazo nyota huyo anaweza akazikosa, ni kuanzia ya Juni 18, itakapocheza na Fountain Gate, kisha kuhitimiza msimu huu kwa kucheza na Tabora United Juni 22, zote zikicheza kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Coastal Union, Abbas Elsabri alisema mchezaji huyo amepewa mazoezi binafsi kutokana na majeraha aliyokuwa nayo, hivyo suala la kucheza mechi mbili zilizobakia kwa sasa ni ngumu.
“Ni ngumu kucheza kwa sababu baada ya kuumia katika mechi yetu na Singida Black Stars, alijiumiza tena goti lake sasa ukiangalia kwa mustakabali wa aina hiyo unaona ni ngumu benchi la ufundi kumtumia licha ya umuhimu wake,” alisema Abbas.
Maabad alijiunga na kikosi hicho Julai 11, 2022, akitokea KVZ FC ya Zanzibar na alikuwa pia mfungaji bora mara mbili mfululizo, akianza na msimu wa 2020-2021, alipofunga mabao 17, kisha na msimu uliofuata wa 2021-2022, akafunga mabao 21.
Licha ya rekodi hiyo bora kwake, ila tangu amejiunga na Coastal Union hajawahi kufikisha hata mabao 10 ya Ligi Kuu Bara, kwa sababu msimu wake wa kwanza wa 2022-2023, alifunga mabao manne na msimu uliopita wa 2023-2024, alifunga matatu tu.
Msimu huu wa 2024-2025, tayari nyota huyo amefunga mabao matano, huku bao la mwisho kufunga lilikuwa la ushindi wa timu hiyo wa mabao 2-1, dhidi ya JKT Tanzania, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Februari 7, 2025.