Saido aanza Geita Gold, Minziro apangua watatu

HATIMAYE leo Saido Ntibazonkiza anaanza katika kikosi cha kwanza cha Geita Gold kinachocheza dhidi ya Singida Big Stars muda mfupi ujao baada ya kukwama kwenye michezo iliyopita kutokana na kukosa vibali vya kazi.
Ntibazonkiza amejiunga na Geita Gold msimu huu baada ya kumalizana na Yanga msimu uliopita ambapo anaongoza safu ya ushambuliaji pamoja na Dany Lyanga na George Mpole.
Wakati Saido akirejea baada ya kutatua suala la vibali, Mghana Shawn Oduro naye amejumuishwa kwenye kikosi cha akiba huku Mjapani, Shinoba Sakai akiwa jukwaani.
Mbali na Saido, Kocha Mkuu wa Geita Gold, Felix Minziro amepangua kikosi chake cha kwanza kilichoanza katika mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Hilal Alsahil ya Sudan kwenye Uwanja wa Azam Complex na kupata ushindi wa mabao 2-1.
Katika kikosi hicho, Minziro amewapumzisha mabeki Oscar Masai na Yahya Mbegu na winga Edmund John ambaye anakosekana baada ya kujumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa chini ya miaka 23.
Kikosi cha Geita Gold kinachoanza leo ni Sebusebu Samson, George Wawa, Adeyum Saleh, Bakari Hussein, Kelvin Yondani, Yusuph Kagoma, Suleman Ibrahim, Deusdedith Okoyo, George Mpole, Dany Lyanga na Saido Ntibazonkiza.
Wanaonazia benchi ni Arakaza McAthur, Yahya Mbegu, Shawn Oduro, Amos Kadikilo, Ramadhan Chombo, Raymond Masota, Offen Chikola, Miraji Athuman na Juma Mahadhi.
Mchezo huo unapigwa saa 10 jioni Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.