Wachezaji Tanzania Prisons wakuna vichwa

Muktasari:
- Tanzania Prisons iliyomaliza ligi nafasi ya 13 na pointi 31, itacheza dhidi ya Fountain Gate mechi za playoff na mshindi wa jumla anabaki ligi kuu, huku atakayepoteza atacheza dhidi ya Stand United kutoka Championship.
WACHEZAJI wa Tanzania Prisons, wamesema baada ya kucheza mechi 30 za Ligi Kuu Bara msimu huu, kwao haijaisha hadi iishe michezo ya mtoano ‘playoff’ ambayo imeshikilia hatma ya kuwepo kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao huku wakiweka mikakati ya ushindi.
Tanzania Prisons iliyomaliza ligi nafasi ya 13 na pointi 31, itacheza dhidi ya Fountain Gate mechi za playoff na mshindi wa jumla anabaki ligi kuu, huku atakayepoteza atacheza dhidi ya Stand United kutoka Championship.
Kiraka wa timu hiyo, Lambart Sabiyanka ambaye anamiliki mabao mawili kwenye ligi msimu huu, alisema:
“Bado tunaendelea na mapambano hadi tone la mwisho kuhakikisha timu inashiriki Ligi msimu ujao.”
Kwa upande wa kiungo wa timu hiyo, Haruna Chanongo ambaye amefunga mabao manne akijiunga na timu hiyo usajili wa dirisha dogo, alisema ni CV mbaya kwa mchezaji kushusha timu, hivyo yupo tayari kutoa nguvu yake kuipambania katika mechi dhidi ya Fountain Gate.
“Kila mchezaji anatamani kujitoa kwa kadiri atakavyoweza ilimradi tuweze kusalia Ligi Kuu, itakuwa mechi ngumu kwani tunakabiliana na timu iliyo na wachezaji wazuri kama Dickson Ambundo na William Edgar,” alisema.
Kauli yake ilikwenda sambamba na ya mshambuliaji wa timu hiyo Jeremiah Juma mwenye bao moja aliyesema:
“Haukuwa msimu mzuri kwetu, ila kama wachezaji tumepambana na tunaendelea kupambana hadi tone la mwisho.”
Meneja na nahodha wa zamani wa timu hiyo, Benjamin Asukile alisema kucheza mtoano ni mara ya pili kwake, akiwa mchezaji msimu wa 2022/23 baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar jumla ya mabao 3-1 walicheza na JKT Tanzania ikiwa Championship ndiyo iliyoamua wabakie salama.
“Naamini siku zote haijaisha hadi iishe, wachezaji wanapaswa kujua siyo mchezo wa ufundi bali unahitaji matokeo ya ushindi na kutumia nafasi kwa usahihi, kwetu ni fainali ambayo kila mchezaji anapaswa kujitoa kwa moyo,” alisema.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Tanzania (TPLB), mchezo wa kwanza wa playoff utachezwa Juni 26, 2025 kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara ambapo Fountain Gate itakuwa mwenyeji, kisha marudiano ni Juni 30, 2025, Tanzania Prisons ikiwa nyumbani Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Timu itakayokuwa na matokeo mazuri kwa jumla, itabaki ligi kuu kwa msimu ujao, itakayopoteza itakwenda kuikabili Stand United.
Stand United iliyoshinda playoff ya Championship kupanda ligi kuu dhidi ya Geita Gold, itaanzia nyumbani Julai 3, 2025, kisha kumalizia ugenini Julai 5, 2025 kusaka nafasi ya kucheza tena Ligi Kuu Bara msimu ujao tangu iliposhuka daraja msimu wa 2018-2019.