SAFARI YA MIAKA 60 KISOKA: Zanzibar ya boli usiichukulie poa kabisa

KWA mashabiki wa kizazi cha sasa ni ngumu kuwaambia na kukuelewa kuwa, timu za visiwa vya Zanzibar, zilikuwa zikitetemesha katika soka la kimataifa.

Unajua kwanini? Hii ni kwa sababu kwa miaka ya hivi karibuni timu za visiwani humo zinazoshiriki michuano ya CAF zimekuwa ‘nyoronyoro’ mno kiasi ni ngumu kuvuka mechi za mchujo ili kuingia hatua ya makundi.

Utabisha nini, wakati msimu huu tu timu za visiwa hivyo yaani Kipanga na KMKM zimejikuta zikikwama kuvuka makundi kutokana na kunyooshwa na wapinzani wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

KMKM iliyoshiriki Ligi ya Mabingwa ilitolewa raundi ya kwanza na St George ya Ethiopia, wakati JKU iliyocheza Kombe la Shirikisho Afrika iling’olewa pia kwenye raundi ya kwanza na Singida Big Stars.

Hata hivyo, kwa wasiojua ni kwamba miaka ya nyuma klabu kutoka Zanzibar zilifunika kwelikweli kwenye michuano ya CAF.

Wakati visiwa hivyo vikianza safari ya kuadhimisha Miaka 60 tangu ilipopata Uhuru kutoka kwa koloni la Uingereza Desemba 10, 1963 kabla ya kufanya Mapinduzi Januari 12, 1964, Mwanaspoti linakupa dondoo chache namna visiwa hivyo vilivyoweza kutisha katika soka la ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Afrika kwa ujumla kiasi cha kuweza kusajili nyota wa kigeni kutoka mataifa mengine yakiwamo ya Ulaya.


JKU YAFUNGUA PAZIA

Vinara wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), JKU ndio ilikuwa klabu ya kwanza kutoka Zanzibar kushiriki michuano ya CAF ikicheza Kombe la Washindi mwaka 1975 ikiwa ni miaka 12 tangu nchi hiyo ipate uhuru, hata hivyo haikuweza kufanya vyema kwa kutolewa raundi ya kwanza kwa aibu.

JKU iling’oka kwenye hatua hiyo kwa kufungwa jumla ya mabao 6-1 na Mufulira Wanderers ya Zambia iliyoshinda mechi ya kwanza kwa mabao 3-0 kisha 3-1.

Hata hivyo, rekodi tamu ni pale KMKM ilipokuwa timu ya pili ya visiwani kucheza michuano hiyo mwaka 1978 na kufanikiwa kufika hadi robo fainali, lakini ikajitoa ilipokuwa ikijiandaa kuvaana na Mufulira, kwani awali iliifumua Simba Sc ya Uganda kwa mabao 3-1.

Hatua kama hivyo ya robo fainali ya michuano hiyo ilifikiwa na Malindi mwaka 1994 na kutolewa na Mbilinga ya Gabon kwa mabao 4-1, baada ya awali kupenya mbele ya KCCU Uganda iliyotolewa na CAF kisha kuifunga Eleven Men in Flight ya Eswatini (Swaziland ya zamani) kwa jumla ya mabao 2-0.


MALINDI BALAA

Kuonyesha kuwa Malindi hawakubahatisha kufika robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika, wababe hao wa Zanzibar waliboresha rekodi yao kwenye michuano ya CAF kwa kufika nusu fainali ya Kombe la CAF (ambayo iliunganishwa na ile ya Washindi mwaka 2004 na kuzaliwa Kombe la Shirikisho Afrika la sasa).

Ikiwa chini ya udhamini wa mfanyabiashara maarufu visiwani humo aliyekuwa na kichaa cha soka, Mohammed Naushad, Malindi ikiundwa na mseto wa wachezaji kutoka visiwani humo, Tanzania Bara, Zambia na Bulgaria, ilitetemesha soka la Afrika kwa soka tamu na matokeo mazuri uwanjani.

Ikiongozwa na kina Amour Aziz, Ali Bushir ‘Benitez’, Wazir Seif, Mzambia Maldon Malitoli, Julian Albertov kutoka Bulgaria, Rashid Salim ‘Tall’, Edibily Lunyamila, Nico Bambaga, Victor Bambo, Abdul Malaika na wakali wengine ilianza michuano ya Kombe la CAF mwaka 1995 kwa kuichapa Mbabane Swallows ya Eswatini kwa mabao 3-0 katika raundi ya kwanza kabla ya kuitupa nje KCC Uganda pia kwa mabao 3-0 na kutinga robo fainali.

Katika robo fainali iliitupa nje OC Agaza ya Togo kwa mabao 2-0 na kutinga nusu fainali rekodi kubwa pekee kwa timu za Zanzibar katika michuano ya CAF kwa klabu na kukutana na kigingi kutoka kwa Etoile du Sahel ya Tunisia iliyotoka nao sare ya 1-1 katika mechi zote mbili na kulazimika kupigiana penalti.

Kwenye hatua hiyo ya penalti, ndipo wanaume hao wakafungwa 4-3 na kushindwa kufikia rekodi ya Simba iliyocheza fainali katika michuano hiyo mwaka 1993.

Naushad aliyefariki dunia na kuzikwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Oktoba, 2021 alilichangamsha soka la Zanzibar enzi za uhai wake kwa kuweka fedha za maana na kuleta majembe ya maana na kusababisha klabu nyingine kufuata nyayo za kuleta nyota waliofanya visiwa hivyo kutisha.


MLANDEGE WAMO

Mwaka 1998 ulikuwa mwaka wa kishindo kwa Mlandege kama ilivyokuwa kwa KMKM miaka ya 1985 ilipotisha Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na Afrika kwa ujumla kwa kutamba kwenye michuano ya Kombe la Kagame.

Mlandege ilikuwa timu ya kwanza kufika fainali ya Kagame mwaka huo na kuvaana na Rayon Sports ya Rwanda na kufungwa mabao 2-1.

Mbali na Mlandege, lakini timu kama Small Simba, Polisi Zanzibar, Miembeni, Kipanga, KVZ ni kati ya timu ambazo zimepeperusha bendera ya Tanzania kwa upande wa Zanzibar kwenye michuano ya CAF, hata kama baadhi ziliishia njiani kwa kupewa vipigo vya aibu kama kilichoikumba Polisi mwaka 2002 ilipofungwa jumla ya mabao 9-0 na CS Hammam Life ya Tunisia.

Kabla ya kipigo hicho kwenye raundi ya pili ya Kombe la Washindi, Polisi iliing’oa Guna Trading ya Ethiopia kwa mabao 2-1 na kukumbana na dhahama hiyo iliyosababisha timu hiyo kubatizwa jina la ‘Wazee wa Tunisia’.


ZILITISHA HADI BARA

Kabla ya kufutwa kwa michuano ya Ligi Kuu ya Muungano iliyoasisiwa mwaka 1982, timu za Zanzibar zilizitetemesha timu za Bara zikiwamo Simba na Yanga kutokana na soka la ushindani na vipaji vya wachezaji kutoka visiwani humo kukimbiza enzi hizo.

Klabu kama Small Simba, Black Fighers, KMKM, JKU, Malindi, Kikwajuni, Mlandege na nyingine zikiwa na nyota wa visiwa hivyo na wengine kutoka Bara kama kina Innocent Haule, Nassor Mwinyi ‘Bwanga’, Malale Hamsini, Athanas Michael, Ali Kibichwa, makipa Ali Bushir, Riffat Said, Hassan Wembe, Seif Bausi na wengine walikuwa wakizitia tumbo joto timu za Bara kabla ya ligi kufutwa mwaka 2003 baada ya visiwani hivyo kutambuliwa rasmi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Hivyo wakati Zanzibar ikijiandaa kuadhimisha Miaka 60 ya Uhuru, mashabiki wa soka wa visiwani humo wana kila sababu ya kujivunia mafanikio yaliyopatikana miaka ya nyuma na kujipanga kwa ajili ya kurejesha makali kwani vipaji bado vipo tele kipindi hiki cha Awamu ya Nane ya Dk Hussein Ali Mwinyi.