Prime
Sababu za mechi ya marudiano kupigwa Zenji

Muktasari:
- Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Jumamosi ijayo na awali ilikuwa ilikuwa ipigwe Kwa Mkapa na wenyeji Simba walishaanza kuuza baadhi ya tiketi kabla ya taarifa iliyotolewa na CAF, sasa ngoma hiyo itachezwa New Amaan kama ilivyokuwa nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Sauzi.
TAARIFA mbaya kwa Simba ni Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limeuondoa mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Bekrane kutoka Uwanja wa Benjamin Mkapa hadi New Amaan, Zanzibar.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa Jumamosi ijayo na awali ilikuwa ilikuwa ipigwe Kwa Mkapa na wenyeji Simba walishaanza kuuza baadhi ya tiketi kabla ya taarifa iliyotolewa na CAF, sasa ngoma hiyo itachezwa New Amaan kama ilivyokuwa nusu fainali dhidi ya Stellenbosch ya Sauzi.
Taarifa ambayo Simba imeshaipokea ni CAF imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanza kuhamisha maandalizi yote ya fainali hiyo ya pili kwenye Uwanja wa Mkapa na sasa yahamie New Amaan, Zanzibar. Hata hivyo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally aliliambia Mwanaspoti jijini hapa jana, kwa sasa uongozi unajikita zaidi kwa mechi ya ugenini na baada ya hapo itatoa taarifa rasmi kwa ajili ya pambano la marudiano la nyumbani litakalopigwa wikiendi ijayo ya Mei 25.
“Tumepokea taarifa hiyo na maelekezo niliyoelekezwa na viongozi wangu niwaambie ninyi wanahabari na wanasimba kwa jumla, kwa sasa akili yenu ipo katika maandalizi ya mechi ya ugenini, baada ya hapo, tutawaambia mustakabali wa mechi ya Mei 25,” alisema jana Ahmed.
Taarifa ya kuhamishwa kwa mechi hiyo ya marudiano ya fainali, imekuwa ni kama pigo kubwa kwa Simba ambayo ina rekodi kubwa ya ushindi kwenye Uwanja wa Mkapa kwani ya mwisho kupoteza uwanjani hapo ni Machi 29, 2024 ilipolala 1-0 mbele ya Al Alhy ya Misri robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.
Inaelezwa maofisa wa CAF wanaosimamia ukarabati wa viwanja vitakavyotumikwa kwa ajili ya fainali za Mabingwa wa Kombe la Afrika (CHAN) 2025 inayoandaliwa kwa ushirikiano baina ya nchi tatu za Afrika Mashariki, yaani Tanzania, Kenya na Uganda wameona fainali haistahili kupigwa hapo.
Tukio la uwanja kujaa matope wakati wa robo fainali ya marudiano ya Simba na Al Masry ya Misri iliyong’olewa kwa pelanti baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 ndio yaliyohamisha nusu fainali na hata kwa fainali hiyo, licha ya awali serikali inayoumiliki kusema kila kitu kilikuwa sawa.
Hata hivyo, taarifa nyingine ambazo Mwanaspoti imezipata jana jioni ni mabosi wa Simba na TFF walikuwa wakiendelea kupambana kubadilisha uamuzi huo wa CAF kwa maombi maalum juu ya mechi hiyo ya kihistoria, lakini huenda wakapata ugumu kwani msimamo huo umegusa viwanja vyote.
Hata Amaan ni moja ya viwanja vitakavyotumika kwa fainali hizo za CHAN zitakazofanyika Agosti mwaka huu baada ya kuahirishwa Februari, lakini wakaguzi wa CAF wameona uwanja huo umekamilika ndio maana mechi hiyo imepelekwa huko kama ile ya nusu fainali dhidi ya Stellenbosch.
Sio Simba pekee iliyotibuliwa na CAF, kwani mapema wiki iliyopita Shirikisho hilo, lilizuia Uwanja wa Nyayo, uliopo Kenya kutumika kwa pambano la Dabi ya Mashemeji kati ya AFC Leopards na Gor Mahia ikihofia uwanja huo kuharibika kwa matumizi ya fainali hizo za CHAN.
CAF imekuwa kwenye usimamizi mkubwa wa viwanja hivyo, kutokana na bado vinaendelea na maboresho kwa matumizi ya Fainali hizo za CHAN na baadaye AFCON.
Katika barua iliyosainiwa juzi Mei 14 na Katibu Mkuu wa CAF, Veron Mosengo Omba inaeleza watu uamuzi huo umetokana na majadiliano ya muda mrefu baina ya CAF, TFF na serikali ya Tanzania kwa vile mechi inapigwa kipindi hiki cha mvua, ndiyo sababu ya kuhamisha mechi hiyo Amaan kiufundi.