RS Berkane yatua ikiingiwa ubaridi

Muktasari:
- Kocha mkuu wa Berkane, Mtunisia Mouin Chaabani na nahodha wa timu hiyo, Issoufou Dayo, raia wa Burkina Faso, walizungumza mara baada ya kutua visiwani, wakionyesha kutambua ukubwa wa kazi inayowasubiri licha ya ushindi wa 2-0 walioupata katika mechi ya kwanza nyumbani Morocco.
WAKATI joto la fainali ya marudiano ya Kombe la Shirikisho la CAF likizidi kupanda Zanzibar, kikosi cha RS Berkane ya Morocco kimetua salama nchini, huku kikiwa na presha ya mechi ya Jumapili dhidi ya Simba itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Kocha mkuu wa Berkane, Mtunisia Mouin Chaabani na nahodha wa timu hiyo, Issoufou Dayo, raia wa Burkina Faso, walizungumza mara baada ya kutua visiwani, wakionyesha kutambua ukubwa wa kazi inayowasubiri licha ya ushindi wa 2-0 walioupata katika mechi ya kwanza nyumbani Morocco.
"Tumecheza dhidi ya timu yenye uzoefu mkubwa, hata katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Tulitengeneza nafasi na tuliweza kuwabana sana nyumbani kwetu, lakini bado kazi haijaisha," alisema Chaabani huku akisisitiza kuwa mashindano haya hayana uhakika hadi dakika ya mwisho.
Kocha huyo alisema hawafurahii sana ushindi huo wa awali kwani wanajua mazingira ya ugenini, hasa dhidi ya Simba mbele ya mashabiki wao wenye hasira ya kulipa kisasi. "Simba ni timu yenye uwezo mkubwa. Tunajua kuwa Amaan watakuja tofauti, na tutahitaji nidhamu ya hali ya juu," aliongeza kwa msisitizo.
Katika mechi ya kwanza, Berkane ilitumia dakika 14 tu kufunga mabao yote kupitia Mamadou Camara na Oussama Lamlaoui, lakini Chaabani alikiri kuwa walikosa nafasi kadhaa ambazo zingewapa nafasi nzuri zaidi kuelekea marudiano.
"Lengo letu kubwa sasa ni kuhakikisha tunapata bao la ugenini. Bao moja linaweza kubadilisha kila kitu. Tunapaswa kuwa makini dakika zote," aliongeza kocha huyo wa zamani wa Esperance ya Tunisia.
Kwa upande wa nahodha Dayo, ambaye ni miongoni mwa wachezaji wenye uzoefu mkubwa barani Afrika, alionekana kuwa na mtazamo wa tahadhari zaidi. "Tulifunga mabao mawili, lakini tulihitaji hata la tatu ili kujihakikishia zaidi. Fainali huwa ngumu, na kila kosa linaweza kugharimu kikosi chote," alisema beki huyo mahiri.
Dayo alisema wanatambua mazingira ya Zanzibar hayatakuwa mepesi, hasa kwa kuwa Simba itaingia kwa hamasa kubwa ya kutafuta bao la mapema. "Tutacheza mbele ya mashabiki wengi wa Simba, na hiyo ni changamoto nyingine. Lakini tuna imani na timu yetu, tuna uzoefu wa kucheza katika presha kama hii," alisema kwa utulivu.
Kauli hizo kutoka kwa benchi la ufundi na wachezaji wa Berkane zinaonyesha jinsi walivyojipanga kwa tahadhari kubwa, wakitambua kwamba Simba ina historia ya kufanya maajabu katika mechi za nyumbani, hasa kwenye mechi za hatua ya mtoano za kimataifa.
Kwa Simba, ushindi wa mabao matatu bila majibu utatosha kuwapa taji lao la kwanza la CAF, lakini kwa Berkane, bao moja tu linaweza kuwavuruga kabisa Wekundu wa Msimbazi katika ndoto yao.