Beki Coastal Union amtaja Pacome

Muktasari:
- Viva ambaye aliwahi kuichezea Malindi ya Ligi Kuu Zanzibar, alisema hana shaka kuwa Zouzoua ni tofauti na viungo wengi waliopo ligi kuu kwa sasa kutokana na uwezo wake wa kupenya kati ya safu ya ulinzi na kusaidia timu yake kutengeneza nafasi.
BEKI wa kati wa Coastal Union na timu ya Taifa ya Zanzibar, Abdallah Denis ‘Vivaa’, ametamka wazi kuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua, ndiye mchezaji hatari zaidi kwa sasa Ligi Kuu Bara.
Viva ambaye aliwahi kuichezea Malindi ya Ligi Kuu Zanzibar, alisema hana shaka kuwa Zouzoua ni tofauti na viungo wengi waliopo ligi kuu kwa sasa kutokana na uwezo wake wa kupenya kati ya safu ya ulinzi na kusaidia timu yake kutengeneza nafasi.
“Kwa maoni yangu binafsi kama beki ambaye nimekabiliana naye uwanjani, Pacome, ni kiungo hatari mno. Ana kasi, anajua wakati gani wa kupiga pasi, wakati gani wa kupenya. Ni mmoja wa wachezaji ambao ukimpa nafasi moja tu, anakuharibu,”€ alisema Viva.
Zouzoua ambaye huu ni msimu wake wa pili akiwa Yanga SC, ameonyesha kiwango cha juu na kuwa mmoja wa wachezaji wa kuaminiwa ndani ya kikosi hicho chini ya makocha tofauti akiwemo Miguel Gamondi.
Kwa mujibu wa takwimu Zouzoua amefunga mabao 12 na kutoa asisti 10, hivyo kuwa na mchango wa moja kwa moja kwenye mabao 22 ya Yanga msimu uliopita kiasi cha kupigiwa chapuo la kuwa MVP.
Viva alisema licha ya kwamba Ligi Kuu ina viungo wengi wenye vipaji,wachache sana wanaweza kuhimili presha na kuamua mechi kubwa kama anavyofanya nyota huyo kutoka Ivory Coast.
“Wachezaji wengi wana vipaji, lakini si wote wanaweza kubeba timu kwenye mechi kubwa. Zouzoua ana ujasiri wa kuchukua maamuzi magumu na mara nyingi anafanya maamuzi sahihi,” aliongeza.
Beki huyo wa Coastal Union alikiri kuwa kukabiliana na Zouzoua kunahitaji nidhamu na msaada wa pamoja kama timu, kwani ni mchezaji mwenye akili na kasi na aliye na maamuzi ya haraka.
Mbali na sifa hizo, Viva anaamini kuwa mafanikio ya Zouzoua ni matokeo ya utulivu ndani ya Yanga pamoja na maelewano makubwa ndani ya timu, jambo ambalo linamwezesha kucheza kwa uhuru na kuleta madhara.