Nicholas Gyan aingia anga za Pamba Jiji

Muktasari:
- Nyota huyo ambaye amecheza kwa mafanikio Simba hajamaliza msimu na timu ya Fountain Gate kutokana na changamoto ya malipo sasa ni mchezaji huru yupo nchini kwao Ghana.
PAMBA Jiji imeonyesha nia ya kunasa saini ya winga wa zamani wa Fountain Gate, Mghana, Nicholas Gyan kwa ajili ya kuwapa huduma yake msimu ujao 2025/26.
Nyota huyo ambaye amecheza kwa mafanikio Simba hajamaliza msimu na timu ya Fountain Gate kutokana na changamoto ya malipo sasa ni mchezaji huru yupo nchini kwao Ghana.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Pamba Jiji, kimeliambia Mwanaspoti mazungumzo baina ya uongozi wa timu hiyo na mchezaji yapo kwenye hatua nzuri na wanaamini mambo yakienda vizuri dili litakamilika.
“Tayari tumeanza kuboresha kikosi chetu, hatuhitaji kuanza kupigana vikumbo na timu nyingine dirisha kubwa la usajili, hivyo naamini muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi ni wachezaji gani wapo mawindoni na wangapi tumemalizana nao,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Usajili unafanyika wakati wowote, masuala ya dirisha la usajili ni kukamilisha kile tulichokifanya kwa mazungumzo kwa kukiweka kwenye makaratasi na kusubiri uthibitisho tumeanza kuzungumza na Gyan ni winga mzuri anaweza kutupa vitu vingi uwanjani kutokana na kuwa na uwezo wa kucheza nafasi nyingi.’
Mtoa taarifa huyo alisema baada ya msimu kukamilika tayari wamepokea ripoti ya kocha na sasa wanapambana kuhakikisha wanaifanyia kazi kwa kusajili wachezaji ambao watakuwa bora na kuongeza ushindani kikosini.
“Ubora wa winga huyo umetuvutia, tumemfuatilia kuanzia tulipocheza naye lakini pia ni mchezaji ambaye tayari amethibitisha ubora wake Ligi Kuu Bara.”
“Hicho kitu kimefanyika na tumeridhishwa na uwezo wake.”