Rais Samia aipa 5 Yanga kufuzu robo fainali CAF

Muktasari:

  • Yanga ilitinga katika hatua hiyo Jumamosi Februari 24 mwaka huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Yanga SC kwa kuifunga CR Belouizdad ya Algeria na kutinga robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilitinga katika hatua hiyo Jumamosi Februari 24 mwaka huu baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ujumbe wa salamu za pongezi kwa Yanga ulioandikwa leo Februari 25 kwenye ukurasa rasmi wa Rais Samia katika mtandao wa Instagram na X (twitter) unasomeka; "Naipongeza Klabu ya Yanga kwa kufanya vyema katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), na kufanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali. Mafanikio haya yameandika historia kubwa kwa klabu na sekta ya michezo nchini. Mmeleta furaha kwa mamilioni ya mashabiki wenu na Watanzania kwa ujumla."

Yanga imeweka historia jana ya kufuzu hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza tangu ilipofuta gundu la miaka 25 na kutinga makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mechi ya kwanza Yanga dhidi ya Belouizdad ilikuwa ni Novemba 24, 2023 na Wanajangwani walipokea kichapo cha mabao 3-0 kwenye Uwanja 5 July 1962, Algeria.

Yanga imefuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa huku ikiwa na mechi moja mkononi ambayo itaikutanisha na vinara na mabingwa mara 11 wa michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika, Al Ahly katika mechi ya kusaka timu itakayomaliza kileleni mwa kundi D lililokuwa pia na timu ya Medeama ya Ghana.